• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Matendo ya Moi yatadumu karne nyingi – Uhuru

Matendo ya Moi yatadumu karne nyingi – Uhuru

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumamosi alisema Rais Mstaafu Daniel Moi atakumbukwa kwa miaka mingi na Wakenya.

Kwenye taarifa kuhusu kifo cha rais huyo wa pili wa Kenya, Rais Kenyatta alisema vitendo vya Moi vilivyobadilisha Kenya havitasahaulika kwa karne nyingi zijazo.

Rais Kenyatta alisema kuwa Moi aliacha kumbukumbu kubwa ya utendakazi mwema, ambayo itakumbukwa na vizazi vingi vijavyo.

“Kumbukumbu ya Bw Moi itadumu daima, kwani inawiana pakubwa na historia ya Kenya. Sisi tulioachwa tunapaswa kudhihirisha uwezo wetu katika kuendeleza ndoto na vitendo vyake,” alisema Rais.

Alitoa ujumbe huo jana kwenye hotuba maalum kutoka Ikulu ya Nairobi.Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kuzungumzia hadharani kuhusu kifo cha Moi, aliyefariki wakati akiwa ziarani nchini Amerika.

Rais aliyeandamana na Naibu Rais William Ruto, mawaziri na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini alisema Moi alikuwa kiongozi aliyefanya maamuzi yaliyofaidi Kenya.

Rais alimsifu Bw Moi kama kiongozi shupavu ambaye alidhihirisha uwezo mkubwa, licha ya kupuuziliwa mbali na baadhi ya wanasiasa kama “wingu la kupita tu.”

Bw Moi alipewa msimbo huo na baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya ambao hawakutaka arithi Mzee Jomo Kenyatta kama rais alipofariki mnamo 1978.

Rais Kenyatta alimtaja Moi kama kiongozi mwenye maono, aliyeheshimiwa nchini, eneo la Afrika Mashariki na barani Afrika kwa jumla.

“Licha ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu mnamo 2002, ambapo nilikuwa mwaniaji urais wa Kanu, Bw Moi aliondoka ofisini kwa hekima,” akasema.

Vile vile alimsifu kama kiongozi aliyeifahamu Kenya kwa undani na kuweka maslahi ya Wakenya mbele.

Baada ya hotuba hiyo, Rais Kenyatta alielekea katika majengo ya Bunge la Kitaifa, ambako aliwaongoza viongozi wengine na Wakenya kuutazama mwili wa Bw Moi.

Rais pia alikutana na familia ya Bw Moi ambapo aliifariji kutokana na kifo chake.Aliandamana na mkewe, Bi Margaret Kenyatta, mamake, Mama Ngina Kenyatta kati ya wengine.

Bw Moi alifariki mnamo Jumanne katika Nairobi Hospital, jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda.Rais Kenyatta alisema Rais huyo wa zamani alikuwa kiongozi mashuhuri aliyetekeleza jukumu kubwa katika kupigania uhuru wa Kenya na kutumia muda mwingi wa maisha yake kuhudumia taifa hili.

“Jua limetua kwa mtu aliyekuwa wa ajabu. Kiongozi mwenye hekima na huruma. Mwanadiplomasia imara. Mtu aliyehudumia taifa kwa ungwana na heshima,” alisema Rais.

Alisema Moi alikuwa mtetezi wa Afrika. “Hadi siku yake ya mwisho mamlakani, alibaki kujitolea na tayari kulinda Afrika na watu wake. Aliamini, kwa dhati, kwamba tuna suluhisho kwa matatizo yaliyokumba bara letu,” akasema Rais.

Awali, mwili wa Bw Moi ulitolewa katika hifadhi ya maiti ya Lee kwa kigari maalum ukisindikizwa na wanajeshi.Wakenya watautazama mwili huo kwa siku tatu; kuanzia jana hadi Jumatatu.

Bw Moi anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru mnamo Jumatano.

You can share this post!

Sababu ya Moi kubeba rungu kila alipoenda

Wakazi wa Nairobi walivyojitokeza kuona mwili wa Moi

adminleo