• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Moi atakavyozikwa kwa heshima ya kipekee

Moi atakavyozikwa kwa heshima ya kipekee

VINCENT ACHUKA na NYAMBEGA GISESA

RAIS wa pili wa Kenya Daniel Arap Moi atazikwa kwa sherehe za aina yake zitakazoongozwa na wanajeshi.

Kutokana na kuwa alikuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Kenya alipokuwa Rais, yeye ni afisa wa hadhi ya juu katika jeshi, na kwa msingi huu mazishi yake yatafanywa kwa mitindo yote ya kijeshi.

Kwa upande mwingine, Mzee Moi pia alikuwa kiongozi wa jamii ya Wakalenjin na mshirika wa Kanisa la Africa Inland Church (AI) hivyo basi, desturi za kabila lake la Tugen na Kikristo pia zinatarajiwa kushuhudiwa kwenye ibada ya mazishi yake kesho na Jumatano mwili wake utakapozikwa.

Kutakuwa na ibada ya wafu ya dini mbalimbali katika uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi kesho.Mwili wa Mzee Moi, ambao unalindwa na wanajeshi kwa saa 24, utapelekwa uwanjani Nyayo na kisha baadaye kwake Kabarak na wanajeshi wa daraja la Meja na wengine wa daraja za juu.

Watakaobeba jeneza pia watakuwa wa daraja hizo.Kaburi mwili wake utakapozikwa pia litachimbwa na wanajeshi.

Mwili wake utakapokuwa ukiwekwa kaburini na wanajeshi, tarumbeta itakuwa ikipigwa. Desturi hiyo inafahamika kama ‘Last Post’ na ilianzishwa na jeshi la Uingereza katika Karne ya 17 kabla ya kuenea katika mataifa ya Jumuiya ya Madola.

Hiyo itakuwa ni ishara ya safari ya mwisho, kumaanisha kazi ya mwanajeshi husika imekamilika na sasa wakati wake wa kupumzika umefika.

Jeneza la Moi, ambalo litafunikwa kwa bendera ya Kenya, litawekewa pia sare yake ya kijeshi, upanga, viatu na kofia.

Ijapokuwa Mzee Kenyatta alipigiwa milio 21 ya bunduki ya heshima wakati wa mazishi yake, Mzee Moi atapigiwa milio 19.

Kulingana na afisa wa jeshi John Muthoka, idadi ya milio hutegemea daraja la mwanajeshi kikosini.

Jukumu hilo litatekelezwa na kikosi cha jeshi la wanamaji, kwa mujibu wa Msemaji wa KDF, Paul Njuguna.

Baadaye, kutakuwa na maonyesho ya ndege za kijeshi kutoka kwa kikosi cha jeshi la wanahewa.

Ni baada ya hapo ambapo familia ya marehemu itapewa bendera ya urais, bendera ya kitaifa kisha wimbo wa taifa utaimbwa.

Gwaride dogo la heshima litakaguliwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa heshima ya Mzee Moi. Maafisa wa ngazi za juu wa jeshi pia wanatarajiwa kutembelea familia ya Moi rasmi, na kuwakabidhi medali za kijeshi zilizokuwa za Mzee Moi.

Wakati wa mazishi ya mke wake Lena mnamo 2004, Mzee Moi alisema angependa kuzikwa kwando yake.

Kutokana na kuwa ni mzee wa jamii ya Watugen, Mzee Moi anatarajiwa kuzikwa kichwa chake kikiwa upande wa mashariki ambako jua huchomoza.

Wakati huo huo, serikali imeweka kila juhudi kumpa Mzee Moi mazishi yanayostahili hadhi yake kama rais aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi.

Dalili zinaonyesha mazishi ya Mzee Moi yatakuwa ya aina yake, na yanaweza tu kufananishwa na yale ya hayati Jomo Kenyatta aliyefariki miaka 42 iliyopita.

Kufikia Ijumaa jioni, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ilikuwa imealika marais wa sasa na wa zamani takriban 30 kutoka mataifa ya nje kuhudhuria mazishi ya Mzee Moi.

Wengine walioalikwa ni mabalozi, wakuu wa tume mbalimbali nchini, wafanyabiashara tajika, wanasiasa na wakuu wa asasi za kiserikali.

Raia wa kawaida pia watakuwa huru kuhudhuria. Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alisema mipango ya kiusalama imekamilika kuhakikisha hakutakuwa na tatizo lolote.

“Kuna polisi wa kutosha Nairobi, Nakuru, Kabarak na katika barabara zote zitakazotumiwa miji hiyo. Wakenya wanaombwa waje kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Rais wakijua watakuwa salama,’ akasema.

Inatarajiwa kuwa watu zaidi ya 200,000 watakuwa wamejitokeza kumpa Mzee Moi heshima za mwisho katika sherehe mbalimbali.

Sherehe hizo ni pamoja na kufariji familia nyumbani kwake Kabarnet Gardens jijini Nairobi, kutazama mwili katika majengo ya Bunge, ibada ya wafu uwanjani Nyayo, ibada ya mazishi katika Chuo Kikuu cha Kabarak na mazishi nyumbani kwake Kabarak.

Wakati wa ibada ya wafu kesho, kutakuwa na televisheni kubwa katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru na nyumbani alikozaliwa eneo la Sacho, Baringo ili kutoa fursa kwa wananchi kufuatilia ibada hiyo.

Viongozi wa makanisa pia watakuwa na fursa ya mahubiri katika maeneo tofauti kabla ya ibada kuu kuanza.

Awali serikali ilikuwa imesema ibada ya wafu itafanyika uwanjani Kasarani kabla ya kutangaza itakuwa Nyayo.

Duru zinasema kwamba mbuzi zaidi ya 1,000 na fahali 200 watachinjwa kwa ajili ya wageni watakaohudhuria mazishi hayo.

You can share this post!

Maziko ya Moi kuibua kumbukumbu za Jomo

Marufuku kwa wabunge wa Ruto kuhutubu kanisani

adminleo