Immaculate Murugi: Serikali ipige jeki filamu nchini
Na JOHN KIMWERE
NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani. Immaculate Murugi hataki kuachwa nyuma, ameibuka miongoni mwa kina dada wanaopania kujizolea umaarufu duniani.
Sura na jina lake si geni kwa wapenzi wa filamu hapa nchini ni miongoni mwa wasanii wanaojivunia kuchota wafuasi wengi tu kupitia kipindi cha ‘Tahidi High’ ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.
Kando na uigizaji binti huyu anamiliki kampuni iitwayo Solutions Media Productions inahusiana na masuala ya uhusiano mwema.
”Nilianza kujihusisha na masuala ya maigizo mwaka 2007 kipindi hicho nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ingawa tangia nikiwa mtoto nilitamani sana kuhitimu kuwa wakili,” anasema na kuongeza kuwa bila kutarajia miaka mitatu baadaye alianza kushiriki uigizaji kwenye kipindi cha Tahidi High akiwa mwigizaji wa ziada.
Anasema katika taaluma ya maigizo amepania kufikia hadhi ya mwigizaji wa Marekani, Ashley Tyler Ciminella maarufu kama Ashley Judd.
Vile vile anasema anataka kuwa produsa pia amiliki kampuni yake ya kuzalisha filamu ili kusaidia waigizaji chipukizi nchini. Kadhalika dada huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa ambazo zilifanikiwa kupata mpenyo na kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini.
Alishiriki filamu kwa jina ‘Changing Times’ ambayo ilionyesha kupitia runinga ya KTN kuanzia mwaka 2010 hadi 2011. Pia alishiriki filamu itwayo ‘Dominas’ iliyopata nafasi kupeperushwa kupitia KBC TV mwaka 2017 hadi 2018.
Pia mrembo huyu anajivunia kufanya kazi na kampuni mbali mbali za kuzalisha filamu kama ‘Spielworks Media,’ ‘K-Youth Productions,’ ‘Moobeam Productions,’ ‘Royal Media’ na ‘Ecila Films’ kati ya zingine.
”Ingawa Wakenya wengi wanapenda filamu za kigeni pia wapo wengine wanaopenda kazi za waigizaji wa humu nchini. Kiukweli Wakenya wenzangu ndio wamefanya niwe nilipo kwa sasa,” alisema na kuwashukuru wafuasi wao kwa kuendelea kuwasapoti kwa kazi zao.
Anadokeza kuwa imekuwa rahisi kupata filamu za kigenini kuliko za hapa nchini. Katika mpango mzima anasema runinga za humu nchini zimezipatia kipau mbele kazi za kigeni hali ambayo imechangia Wakenya wengi kuvutiwa zaidi nazo.
Anasema kuwa hapa nchini angependa sana kufanya kazi na wasanii kama Brenda Wairimu ambaye ameigiza filamu kama ‘Selina’ na ‘Monica.’
Pia yupo Lupita Nyong’o anayetesa si haba katika filamu za Hollywood ambaye amepata umaarufu kwa kazi alizoshiriki kama ’12 Years A Slave’ na ‘Black Panther.’
Dada huyu anasema serikali inastahili kuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono wazalishaji wa humu nchini na kufutulia mbali sheri zinazowakandamiza.
Anasema kando na changamoto zingine sekta ya maigizo nchini ina malipo duni hali ambayo hufanya baadhi ya kusepa na kusaka ajira tofauti.
”Kusema kweli malipo duni ama kutolipwa kabisa hufanya baadhi ya waigizaji chipukizi kuvunjika moyo na kuzipigia chini shughuli za maigizo,” alisema.
Hata hivyo anashauri wenzake kutovunjika moyo upesi licha ya kukutana na pandashuka nyingi katika tasnia ya uigizaji.