• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Inter Milan kileleni mwa jedwali Ligi Kuu ya Italia

Inter Milan kileleni mwa jedwali Ligi Kuu ya Italia

Na MASHIRIKA

MILAN, ITALIA

INTER Milan walitoka nyuma kwa mabao mawili na kukizamisha chombo cha watani wao AC Milan kwa jumla ya magoli 4-2 katika gozi la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) wikendi iliyopita.

Ushindi wa Inter ambao kwa sasa wananolewa na mkufunzi Antonio Conte, uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali baada ya kuwapiku Lazio na mabingwa watetezi Juventus.

Ante Rebic aliwafungulia Milan ukurasa wa mabao kunako dakika ya 40 kabla ya mkongwe Zlatan Ibrahimovic kufanya mambo kuwa 2-0 mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ingawa hivyo, Inter walirejea mchezoni kwa matao ya juu katika kipindi cha pili huku wakifungiwa mabao mawili ya haraka kupitia kwa Marcelo Brozovic na Matias Vecino kunako dakika za 51 na 53 mtawalia.

Ushirikiano kati ya Alexis Sanchez na Stefan de Vrij uliwapa Inter bao la tatu kabla ya Romelu Lukaku kukizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mchuano huo ungalishuhudia idadi kubwa zaidi ya mabao katika dakika za mwisho. Ingawa hivyo, Hakan Calhanoglu na Christian Eriksen wa Inter na Ibrahimovic wa Milan, walishuhudia makombora yao yakigonga miamba ya malango.

Hadi waliposhuka dimbani kwa minajili ya gozi hilo, Milan walikuwa wamepoteza mchuano mmoja pekee kati ya 11 ya awali chini ya mkufunzi wa zamani wa Inter, Stefano Pioli.

Matokeo yao dhidi ya Inter yaliwasaza katika nafasi ya 10 jedwalini kwa alama 32 sawa na Parma na Cagliari.

Kwa upande wao, Inter ambao kwa sasa wanajiandaa kuchuana na Napoli hapo kesho ugenini, hawajapoteza mechi yoyote kati ya 16 zilizopita ligini.

Ushindi dhidi ya Napoli ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 kwa alama 30, utawapa hamasa zaidi ya kuwazamisha Lazio uwanjani San Siro mwishoni mwa wiki hii.

“Ni mapema sana kuanza kuzungumzia kitu ambacho tunaweza tu kukiotea kwa sasa. Muhimu zaidi ni kuzimakinikia mechi zijazo ambazo zitapania kuwatia masogora wangu kwenye mizani. Itakuwa hadi baada ya kusakatwa kwa michuano hii ambapo tutatathmini upya kiwango cha uwezo wetu,” akasema Conte.

Katika mechi nyinginezo za Serie A, Lazio ya kocha Simone Inzaghi iliwanyuka Parma 1-0 katika ushindi uliochangiwa na mvamizi wa zamani wa Man-City, Felipe Caicedo. Ilikuwa ni mechi ya 18 kwa Lazio kupiga bila ya kupoteza hadi sasa msimu huu.

Napoli walipokezwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa Lecce huku Brescia wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Udinese. Sassuolo waliwachabanga Spal 2-1 nao Genoa wakawapokeza Cagliari kichapo cha 1-0.

You can share this post!

ATAHAMA? Bayern Munich tayari kumshawishi Roberto Firmino...

Munala aelezea matumaini tele KCB iko imara

adminleo