• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
NGILA: Usalama mitandaoni unahitaji ushirikiano kimataifa

NGILA: Usalama mitandaoni unahitaji ushirikiano kimataifa

NA FAUSTINE NGILA

UTOVU wa usalama mitandaoni sasa umekuwa janga la kimataifa, huku mataifa yakipoteza matrilioni ya hela kutokana na wizi, udukuzi na uuzaji wa data za siri.

Katika kongamamo la kila mwaka duniani kuhusu suala hili jijini Tel Aviv, Israeli, iliibuka kuwa jinsi teknolojia inavyozidi kukua ndivyo visa vya udukuzi vinaongezeka, na hali hii sasa imefikia viwango vipya kwani majambazi wa mitandaoni sasa wanatumia teknolojia za kipkee kuiba fedha na data za mashirika ya serikali, benki na kampuni.

Katika kongamano hilo nililohudhuria, niligundua kuwa katika kila sekunde, kuna visa 11,000 vya udukuzi kote duniani, hali ambayo inatisha makuzi ya uchumi wa kidijitali.

Na si akaunti za benki, simu au mitandao ya kijamii pekee inayoshuhudia hali hii, mitambo ya kusambaza umeme pia imo hatarini kwani wadukuzi wanaamini kuwa wakidukua na kuchukua usukani wa usambazaji wa umeme, basi watafanya kila watakacho gizani.

Kwenye wasilisho lake kwa maelfu ya wataalamu wa usalama wa intaneti, Waziri wa Kawi nchini Israel Bw Yuval Steinitz alitoa mwito kwa mataifa kutumia teknolojia za kisasa katika kukabili wezi wa mitandaoni.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya usambazaji umeme nchini humo alishauri mataifa kuanza kutumia teknolojia ya blockchain kuzima majaribio ya kudukua mifumo ya umeme, pamoja na kuwapa wakazi bilioni moja waishio bila umeme duniani uhuru wa kutengeneza na kuuza kawi.

Kenya, kwa mfano, ilipoteza sh29 bilioni kutokana na udukuzi hapo 2018, hali inayoanika jinsi mataifa yanayoendelea yalivyolemewa kukabili uovu huo.

Hata hivyo, wataalamu wengi walikubaliana kuwa dunia kwa sasa imekuwa hatari zaidi, hasa mitandaoni, na suluhu ya kudumu ni kushirikiana katika kutoa habari moja kwa moja kwa manufaa ya kila nchi na kampuni duniani.

Ushirikiano huu utayafaidi zaidi mataifa yanayoendelea, kwani yamekosa teknolojia za kisasa na wataalamu waliotimu, na hivyo yanafaa kujitolea kutoa habari zote zinazopata kuhusu mipango ya udukuzi.

Katika ushirikiano huu, Kenya itafaidi pakubwa kwani baada ya kuwekeza mamilioni katika usalama wa mifumo ya kifedha, bado imekuwa ikidukuliwa na hela kuibwa. Mwaka uliopita, tovuti kadhaa za mashirika ya serikali yalidukuliwa, serikali isifanye lolote.

Kwa kupata habari za mbashara kutoka mataifa yenye utaalamu wa kisasa kama Amerika, Ujerumani, Israel, Uchina na Urusi, Kenya itaweza kutibua njama za makundi hatari ya wadukuzi kutoka Iran na Ukraine.

Hata hivyo, kampuni za humu nchini ambazo kulingana na utafiti zimekuwa zikitenga fedha kidogo kujikinga dhidi ya utovu wa usalama katika mifumo ya kidijitali, zitatahitajika kuanza kuipa hali hii kipaumbele katika maamuzi ya usimamizi.

Kuna haja gani uitishwe Sh5 bilioni na wadukuzi ili wakurudishie mfumo wako wa kifedha waliodukua, ilhali una nafasi ya kulipa Sh500,000 kila mwaka upate ulinzi dhabiti dhidi ya uovu huu?

Licha ya kuwa na Sheria ya Data, kampuni za Kenya na serikali zitahitajika kushirikiana na zile za kimataifa kuzuia udukuzi, kwani baadhi ya mbinu zinazotumika na wahalifu wa mitandaoni haziwezi kutambulika kwa kutumia teknolojia zilizopo Kenya kwa sasa.

You can share this post!

Babangu alipenda nyama hasa ya mbavu, Gideon hatimaye...

Ni mavazi ya KANU pekee yataruhusiwa kwa mazishi ya Moi...

adminleo