• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Hatimaye Moi alazwa

Hatimaye Moi alazwa

Na VALENTINE OBARA

RAIS wa pili wa Kenya Daniel arap Moi, hatimaye alizikwa jana katika boma lake eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru kwa heshima za kijeshi.

Maelfu ya watu wa matabaka tofauti walihudhuria ibada ya mwisho ya mazishi iliyofanywa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Kabarak ikiongozwa na Kanisa la Africa Inland Church (AIC) ambalo hayati Moi alikuwa mshirika wake kwa miaka mingi.

Hata hivyo, umma haukuruhusiwa kushuhudia alivyozikwa jana baada ya kuhudhuria ibada ya wafu chuoni Kabarak.

Safari yake ya mazishi ilisimamiwa na Jeshi la Kenya (KDF) ambalo lilihakikisha mipango yote imefanywa kwa utaratibu tangu mwili wake ulipohifadhiwa katika mochari ya Lee jijini Nairobi mnamo Jumanne wiki iliyopita hadi ulipozikwa Kabarak jana.

Katika eneo la mazishi bomani mwake, maombi yalifanywa kisha bendi ya wanajeshi ikapiga tarumbeta za kuaga Amiri Jeshi wao Mkuu wa zamani.

Wanajeshi wa kikosi cha jeshi la wanamaji walifyatua mizinga 19 kwa heshima za hayati Mzee Moi baada ya bendi kucheza wimbo wa taifa.

Hilo lilifuatwa na maonyesho ya ndege kutoka kwa kikosi cha wanahewa ambao waliendesha ndege hizo kwa mtindo wa kipekee unaofahamika kama ‘the missing wingman formation’.

Mtindo huo ni wa kutoa heshima kwa mwanajeshi wa ngazi za juu aliyeaga.

Bendi ya wanajeshi ilipiga tarumbeta zao kwa mara ya mwisho kwa wimbo wa ‘the long reveille’ kabla viongozi wa dini kupewa nafasi kuendesha shughuli ya mwisho ya kufunika kaburi la Mzee Moi.

Familia ilipewa nafasi ya kwanza kurusha mchanga kaburini baada ya viongozi wa dini, wakafuatwa na Rais Kenyatta na mkewe Margret, kisha Naibu Rais William Ruto na mkewe Rachel. Viongozi wengine waliokuwepo walifuata.

Ingawa umri wake rasmi ulisemekana kuwa miaka 94, familia yake ilisisitiza alifariki akiwa na umri wa kati ya miaka 103 na 105.

Hayati Moi ameingia katika historia kama Mkenya wa pili kupewa mazishi ya hadhi ya juu zaidi ya kijeshi baada ya mtangulizi wake Mzee Jomo Kenyatta ambaye alifariki 1978. Hii ni kutokana na kuwa alipokuwa Rais alikuwa pia Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Kenya. Kwa msingi huu, kulifyatuliwa pia mizinga 19 katika mazishi yake jana na tarumpeta kupulizwa.

Mwili wa Moi ulilazwa katika majengo ya bunge la taifa kwa siku tatu kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu wiki hii kutoa fursa ya kutazamwa na wananchi takriban 100,000 waliojitokeza kumtolea heshima za mwisho.

Wakati wa kipindi cha maombolezo tangu wiki jana, bendera ya taifa ilipeperushwa nusu mlingoti kote nchini na katika afisi zote za Kenya nje ya nchi.

Mzee Moi na mkewe marehemu Lena walijaliwa watoto wanane wanaojumuisha wanaume watano na mabinti watatu.

You can share this post!

Uhuru afichua alivyomhepa Moi kwa wiki nzima

Mamia warauka Moi akitoka Nairobi

adminleo