• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mamia warauka Moi akitoka Nairobi

Mamia warauka Moi akitoka Nairobi

 Na CECIL ODONGO

MAMIA ya Wakenya jijini Nairobi, Jumatano walijitokeza katika barababara ya Argwings Kodhek karibu na hifadhi ya maiti ya Lee, mwili wa Rais Mstaafu Daniel Arap Moi ulipokuwa ukiondolewa chumbani humo kusafirishwa Kabarak kwa mazishi.

Kufikia saa 12 asubuhi, Wakenya wengi jijini walioonekana kuwa na huzuni walikuwa wamemiminika katika barabara hiyo ili kushuhudia jinsi Mzee Moi alivyokuwa akiaga jiji la Nairobi.

Wakazi wa Nairobi walipata nafasi kwa siku tatu kuanzia Jumamosi iliyopita, kutazama mwili wa Mzee Moi katika majengo ya bunge.

Jana walijitokeza tena barabarani kuutazama safari yake ya mwisho.

Katika maeneo mbalimbali ya jiji, watu walijitokeza kutazama mwili huo ukisafirishwa kuanzia chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee hadi katika uwanja wa Wilson.

Baadhi ya waliozungumza na Taifa Leo, walisema hiyo ilikuwa fursa yao ya mwisho kuona marehemu Mzee Moi akiondoka sio tu Nairobi, bali kuwapotelea daima katika maisha yao.

Mwili wa Mzee Moi uliondolewa kwenye hifadhi hiyo saa 12.55 asubuhi na kuwekwa kwenye gari la kijeshi. Msafara wake uliokuwa ukisindikizwa na magari kadhaa, pikipiki na maafisa wa polisi, uling’oa nanga saa 1.00 asubuhi.

Watu wa familia ya Mzee Moi nao walikuwa katika basi lililokuwa mbele, huku gari lililobeba mwili wa marehemu ukifuata nyuma ukiwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama.

Msafara huo ulielekea katika uwanja wa ndege wa Wilson kwa chini ya muda usiozidi dakika 15 ikizingatiwa kwamba barabara hiyo ilifungwa na magari ya uchukuzi wa umma yalikuwa yamezuiwa kuitumia kwa muda.

Mwili huo uliwasili uwanjani Wilson na kuingizwa katika helikopta ya kijeshi na ukaondoka Nairobi hadi Kabarak ambako ibada ya mazishi ilifanyika jana. Rais Uhuru Kenyatta aliwaongoza Wakenya kumuaga Mzee Moi wakati wa mazishi hayo.

You can share this post!

Hatimaye Moi alazwa

Wakazi walivyojazana Afraha kufuatilia matukio ya Kabarak

adminleo