Wakazi walivyojazana Afraha kufuatilia matukio ya Kabarak
Na WAANDISHI WETU
MAELFU ya Wakenya ambao hawakupata fursa ya kwenda Kabarak kwa ajili ya hafla ya mazishi ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi, walifuatilia matukio katika Uwanja wa Afraha.
Skrini kubwa za runinga ziliwekwa uwanjani humo kuwezesha wakazi wa Nakuru kufuatilia matukio moja kwa moja kutoka Kabarak nyumbani kwa Mzee Moi.
Serikali ilikuwa imeahidi kuweka skrini kubwa mjini Nakuru na Baringo kuwezesha wakazi kufuatilia hafla ya mazishi.
Malango ya uwanja wa Afraha yalifunguliwa alfajiri na waombolezaji wakaanza kufika na kuketi huku wakingojea hafla ya mazishi kuanza.
Maafisa wa polisi wakishirikiana na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) walidumisha usalama uwanjani hapo.
Kufikia saa tatu asubuhi, uwanja ulikuwa umejaa na waombolezaji waliketi kimya wakingojea kuanza kwa programu katika uwanja wa Kabarak.
Bw Paul Njuguna, mkazi wa eneo la Bondeni alipongeza serikali kwa kuwawekea skrini uwanjani hapo kufuatilia matukio kupitia runinga.
“Nilijua huko Kabarak kungekuwa na msongamano wa watu, hivyo, niliamua kuja hapa moja kwa moja. Nashukuru serikali kwa kujali watu ambao hakuweza kwenda Kabarak,” akasema.
Naye Bi Ann Wambui, alisema kuwa alifika uwanjani hapo kama ishara ya kumuaga Mzee Moi, aliyeongoza Kenya kwa unyenyekevu na upendo.”
Kulingana naye, Mzee Moi alihudumia Wakenya wote kwa usawa bila ubaguzi wa kikabila na anafaa kuigwa na viongozi wote.
“Nilimwona Rais Moi kwa mara ya kwanza huko Nyandarua alipokuja kutoa hatimiliki za mashamba. Nimekuja hapa kushuhudia uongozi wake bora,” akasema Bi Wambui.
Bw Kiben Towett, 67, ambaye ni mkazi wa Rhonda alisema kuwa atakumbuka Mzee Moi kwa mchango wake katika kuboresha elimu.
“Alikuwa mcha Mungu. Tulikuwa tumekariri taarifa za habari kila Jumapili kuhusu Rais Moi akiwa kanisani,” akasema.
“Mzee alipenda mazingira na alihimiza watu kupanda miti. Hakika nina mengi ya kuwaeleza wanangu kuhusu uongozi wa Rais Moi, haswa maziwa ya Nyayo,” akasema Bw Towett.
Hata hivyo, hafla ya mazishi uwanjani hapo yalikuwa mavuno kwa wachuuzi.
Bw Bernard Meigo alisema kuwa alijipatia riziki kwa kuuza vibandiko vilivyokuwa na picha ya Mzee Moi.
“Nilikuwa nauza kibandiko kimoja kwa Sh50. Biashara ilinoga sana kwani niliuza vibandiko vyote,” akasema Bw Meigo.
Bi Joyce Atieno alikuwa akiuza mayai yaliyowasaidia waombolezaji kupunguza makali ya njaa wakifuatilia matukio kwenye skrini.
“Nilifahamu kuwa hata kuangalia runinga kunahitaji nguvu. Hiyo ndiyo maana nilikuja na mayai kuwauzia waombolezaji,”akasema.
Wakazi walifuatilia matukio kutoka Kabarak kutoka asubuhi hadi jioni bila hitilafu yoyote.
Ripoti Za Mercy Koskey, John Njoroge Na Joseph Openda