• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Bayern itanyoa Chelsea katika Uefa – Ballack

Bayern itanyoa Chelsea katika Uefa – Ballack

Na MASHIRIKA

BERLIN, Ujerumani

ALIYEKUWA kiungo mahiri wa Bayern Munich, Michael Ballack, anapigia upatu mabingwa hao wa Ujerumani kutinga robo-fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ballack alipata ufanisi mkubwa akichezea Bayern na pia Chelsea ya Uingereza.

Klabu zake hizo mbili za zamani zitakutana kwa mechi ya mkondo wa kwanza katika raundi ya 16 ya UEFA, itakayochezewa ugani Stamford Bridge, Jumanne ijayo.

Ballack asema Bayern ina nafasi kubwa dhidi ya wapinzani wao, ambao wananolewa na rafiki yake mkubwa Frank Lampard.

Chelsea, ambao walimaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi H, nyuma ya Valencia, walifanikiwa kusonga mbele baada ya kupiku Ajax, waliotinga nusu-fainali msimu uliopita.

Bayern, kwa upande wake, walishinda mechi zao zote za makundi na kusonga mbele bila shida.

“Bayern wana nafasi kubwa kutokana na uzoefu wa muda mrefu. Pia kiwango cha wachezaji wake kiko juu. Isitoshe, kwa sasa Bayern wametulia kuliko walivyokuwa msimu uliopita,” Ballack alisema.

“Ingawa hivyo, Chelsea imesajili vijana wengi ambao hawawezi kupuuzwa. Kikosi kinaundwa na wachezaji wengi wa umri mdogo lakini hodari mno, hasa wanapokuwa karibu na eneo la hatari. Changamoto ni kwamba Lampard ni mpya katika kazi yake, hali ambayo inaipa Bayern nafasi kubwa.”

Kabla ya pambano hili wiki ijayo, Chelsea itakutana na Manchester United Jumatatu usiku – siku moja tu baada ya Bayern kukabiliana na Cologne katika mechi ya Bundesliga.

Wakati huo huo, refarii wa soka nchini Italia amepigwa marufuku ya mwaka mmoja, baada ya kumshambulia mlinda lango wakati wa mechi ya ligi ya daraja la chini.

Shirika la habari la Ansa liliripoti kwamba, mnamo Februari 1 mwamuzi Antonio Martiniello alimtimua Matteo Ciccioli wa klabu ya Borgo Mogliano, ilipokuwa ikicheza na Montottone katika eneo la Macerata Mashariki.

Wenyeji walishinda 3-1.

Baada ya mechi kumalizika kipa huyo aliondoka uwanjani akielekea katika chumba cha kubadilisha nguo, lakini huko akapatana na refa Martiniello ambaye alimkabili.

Fujo zilizuka baada ya mwamuzi huyo kumtupia makonde kipa Ciccioli, ambaye alilazimika kukimbizwa hospitalini apewe tiba.

Marufuku dhidi ya Martiniello inamzuia kuchezesha mechi yoyote, na pia kuhudhuria mechi yoyote katika taifa la Italia, iwe ya ligi ya kulipwa ama mashindano madogo.

Mkuu wa polisi wa eneo la Macerata alisema adhabu hiyo ilifaa kwani Martiniello alikosa kuonyesha mfano mwema.

You can share this post!

Jose Mourinho awakasirisha Man-United

Jowie aachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa taslimu

adminleo