HabariSiasa

Sonko ajipeleka kichinjioni

February 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

HATUA ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko kumteua Anne Kananu Mwenda kuwa naibu wake, imegeuka kuwa kamba aliyowarushia mahasimu wake kumnyonga nayo.

Hii ni baada ya kuibuka kuna njama ya kumtimua mara Bi Mwenda akiidhinishwa.

Tayari madiwani wa bunge la Nairobi wanaompinga Bw Sonko wameandaa hoja ya kumtimua mamlakani na wanasubiri mchakato wa kuidhinisha Bi Mwenda ukamilike ndipo wamvue ugavana.

Kiranja wa wachache Peter Imwatok, ambaye ni mkosoaji wa Bw Sonko, anasema mswada wa kumtimua uko tayari na wanasubiri wakati muafaka wa kuuwasilisha katika bunge la kaunti.

Madiwani hao wanasema wanataka kuiga wenzao wa Kiambu ambao walimtimua Bw Fedinard Waititu anayekabiliwa na mashtaka ya ufisadi sawa na Bw Sonko.

Bw Waititu na Bw Sonko walipigwa marufuku kukanyaga ofisi zao hadi kesi zinazowakabili zitakapoamuliwa.

Nafasi ya Bw Waititu ilichukuliwa na naibu wake James Nyoro ambaye aliapishwa siku moja baada ya Seneti kuidhinisha kutimuliwa kwake. Mchakato wa kutimua Bw Waititu uliungwa mkono na mirengo ya Rais Uhuru Kenyatta katika Jubilee na chama cha ODM chake Raila Odinga.

Tofauti na Kiambu, Nairobi haina naibu gavana baada ya nafasi hiyo kuachwa wazi na Polycarp Igathe aliyejiuzulu 2018 baada ya kutofautiana na Bw Sonko.

Bw Sonko amekuwa akiongoza bila naibu hadi Januari 6 mwaka huu alipomteua Bi Mwenda na kuwasilisha jina lake kwa Spika Beatrice Elachi wa bunge la kaunti.

Awali Bi Elachi alikataa uteuzi huo akisema Bw Sonko hakufuata utaratibu unaohitajika. Lakini baadaye aliwasilisha jina la Bi Mwenda kwa kamati ya uteuzi ya bunge la kaunti ili imkague kulingana na sheria.

Duru zinaeleza Bi Elachi alibadilisha msimamo kutokana na ushauri kutoka kwa ngazi za juu serikalini.

Mnamo Jumatatu wiki hii, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliidhinisha Bi Mwenda na hivyo kutoa nafasi kwa kamati ya uteuzi ya bunge la kaunti kumpiga msasa.

Duru katika bunge la Nairobi zinasema mchakato wa kumuidhinisha Bi Mwenda utaharakishwa ili kujaza nafasi ya naibu gavana, na hivyo kutoa nafasi ya kumtimua Bw Sonko.

“Mipango imekamilika, tunasubiri nafasi ya naibu gavana ijazwe ili tusonge mbele. Nairobi itakuwa na usimamizi mpya kabla ya Machi mwaka huu,” alisema diwani mmoja wa chama cha Jubilee ambaye hakutaka tutaje jina lake.

Alisema mipango ya kumbandua Bw Sonko ulisitishwa mwaka 2019 ili kuepusha mgogoro wa uongozi iwapo Bw Sonko angetimuliwa bila naibu wa kuchukua nafasi yake.

“Kulikuwa na mipango miwili ya kuhakikisha kwamba Sonko harejei ofisini. Wa kwanza ulikuwa ni kumtimua na wa pili ulikuwa ni kuvunja serikali ya kaunti na kuteua kamati ya kuisimamia chini ya Bi Elachi. Hata hivyo, Sonko alipoteua gavana na kufuatia yaliyotendeka Kiambu, iliamuliwa tufuate wa kwanza,” alisema diwani huyo.

Ripoti katika ofisi ya Bw Sonko zilidokeza kuwa aliteua Bi Mwenda ili kusambaratisha mipango ya kuvunja serikali yake na kuteua kamati simamizi.

Hata hivyo, chaguo lake la Bi Mwenda lilirahisisha mpango wa mahasimu wake kwa kuziba pengo ambalo lingezua mzozo wa uongozi iwapo angetimuliwa bila naibu gavana.