Joho hatarini kutupwa ndani miezi 6
NA PHILIP MUYANGA
GAVANA wa Mombasa Hassan Joho yumo kwenye hatari ya kutupwa gerezani kwa miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kupuuza maagizo ya mahakama.
Katika uamuzi wake, Jaji Sila Munyao wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi jijini Mombasa, alimwamuru gavana pamoja na diwani wa Changamwe Bernard Ogutu kufika kortini Machi 3 kujitetea kabla ya kuhukumiwa.
Uamuzi huo unatokana na ombi la mfanyibiashara wa Mombasa, Ashok Doshi na mkewe Pratibha, ambao walikuwa wamelalamika kuwa Bw Joho na Bw Ogutu walikiuka agizo la mahakama lililozuia serikali ya Kaunti ya Mombasa kuingia bila ruhusa katika shamba lao.
“Bw Joho hajakanusha kuwa alikuwa katika ardhi hiyo, na pia hajakana kuwachochea watu waliokuwa hapo kufanya uharibifu uliolalamikiwa,” alisema Jaji Munyao katika uamuzi wake.
“Kuna ushahidi wa kutosha kuwa Bw Joho na Bw Ogutu walizuru ardhi hiyo kinyume na maagizo ya mahakama. Hatua hiyo ilifanya lango kuu kuvunjwa na ukuta uliojengwa na walalamishi kubomolewa,” jaji huyo akasema.
Kupitia wakili Willis Oluga, mfanyibiashara huyo na mkewe walisema kuwa mnamo Mei 10 mwaka jana, maafisa wa serikali ya kaunti wakiongozwa na Bw Joho na viongozi wengine wa Mombasa walivamia ardhi hiyo na kuvunja lango.
Waliongeza kuwa viongozi hao pia walifanya mkutano wa umma ambapo walimshtumu Bw Doshi kuwa mnyakuzi wa ardhi.
“Gavana wa Kaunti ya Mombasa alisema katika mkutano wa umma uliofanyika katika ardhi hiyo kuwa kama ‘rais’ wa Kaunti ya Mombasa alikuwa amefutilia mbali cheti cha umiliki wa ardhi hiyo,” wawili hao waliambia korti.
Bw Oluga alimwambia Jaji Munyao kuwa hakukuwa na hati yoyote ya kiapo iliyokuwa inakanusha madai kuhusiana na Gavana Joho kukiuka maagizo ya mahakama.
Kupitia wakili Murtaza Tajbhai, Bw Joho aliiambia mahakama kuwa hakuwa amepewa agizo hilo la mahakama.
Bw Doshi na mkewe pia wanataka agizo la kudumu la kuzuia serikali ya kaunti na Bw Ogutu au mtu yeyote kuvunja ukuta au nyumba yoyote katika ardhi hiyo.
Wanaongeza kuwa madai ya kuwa ardhi hiyo ilikuwa imenyakuliwa kutoka kwa shule hayana msingi wowote.