• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
Tupewe mamlaka ya kuadhibu wachochezi -NCIC

Tupewe mamlaka ya kuadhibu wachochezi -NCIC

Na WANDERI KAMAU

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) inataka kupewa mamlaka sawa na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili kuwaadhibu wanaopatikana na makosa ya uchochezi.

Tume hiyo ilisema hiyo ndiyo hatua pekee itakayohakikisha kuwa watu ambao wanawachochea wananchi wanachukuliwa hatua za kisheria.

Akiwasilisha mapendekezo yake kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi, mwenyekiti wa tume hiyo Dkt Samuel Kobia alisema hilo litaondoa tashwishi miongoni mwa wananchi kuhusu utendakazi wake.

“Ni sharti Sheria ya NCIC ifanyiwe mageuzi ili kuhakikisha kuwa tunaharakisha taratibu za kuwaadhibu wale wanaopatikana na hatia ya kuwachochea wananchi,” akasema Dkt Kobia.

Tume hiyo imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha taratibu za kuwachunguza wanasiasa na watu wanaopatikana kushiriki katika uchochezi, hasa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Lakini katika kujitetea kwake, imekuwa ikizilaumu mahakama kwa kuchelewesha kesi ambazo inawasilisha kwake.

Nazo mahakama zimekuwa zikiilaumu tume hiyo kwa kutofanya uchunguzi wa kutosha dhidi ya waathiriwa.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamejipata lawamani ni Mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), mwanablogu Cyprian Nyakundi, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama kati ya wengine.

Hata hivyo kesi zao zilifutiliwa mbali na mahakama kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Wengine waliotoa hoja zao ni kamishna wa tume hiyo Bi Wambui Nyutu.

You can share this post!

Alice Wahome amshtaki Matiang’i

Rungu la Moi sasa launganisha ‘vitoto vya kifalme’...

adminleo