Habari

Mabunge ya Kaunti yataka mamlaka zaidi

February 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

BARAZA la Maspika wa Kaunti (CAF) linataka mabunge ya kaunti kupewa mamlaka zaidi na kutengewa fedha zake maalum kama Bunge la Kitaifa na Seneti ili kuyawezesha kujisimamia kwa njia huru.

Hatua hiyo itayawezesha kufuatilia utendakazi wa magavana, bila kutegemea ufadhili wao.

Akiwasilisha mapendekezo yake kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi Ijumaa, mwenyekiti wa baraza hilo Bw Ndegwa Wahome alisema kwamba, licha ya kutegemewa kutekeleza majukumu muhimu kuhusu usimamizi wa serikali za kaunti, huwa wanashindwa kutokana na vikwazo vingi katika utendakazi wao.

“Majukumu mengi tunayotegemewa kufanya huwa yanatuhitaji kutumia fedha, ila huwa tunahitajika kunyenyekea ili kupata pesa hizo kutoka kwa magavana. Hilo limeyafanya mabunge mengi kuzuiwa na magavana kuwachunguza kila wanapotuhumiwa kufuja fedha za umma,” akasema Bw Wahome, ambaye pia ndiye Spika katika Bunge la Kaunti ya Nyandarua.

Alisema kuwa ingawa Hazina ya Kitaifa huwa inayatengea fedha mabunge hayo, huwa zinajumuishwa na fedha za kawaida za matumizi ya kaunti, hali ambayo huifanya vigumu kwao kuzipata.

Baraza pia lilipinga vikali pendekezo la kubuniwa kwa mfumo wa majimbo, likisema kuwa badala yake, serikali inapaswa kuipa nguvu miungano ya kiuchumi ambayo imebuniwa na kaunti mbalimbali.

“Miungano hiyo inastahili kufadhiliwa ili izisaidie kaunti kupiga jeki mipango ya maendeleo,” akasema.

Mbali na hayo, baraza lilipinga vikali pendekezo la kuifanyia mageuzi Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), likisema kuwa haipaswi kuingiliwa kwa vyovyote vile na wanasiasa.

Kwenye ripoti yake iliyozinduliwa mwaka uliopita, jopo lilipendekezaza IEBC kuwa na wawakilishi kadhaa kutoka vyama vya kisiasa nchini.

Lakini CAF inapinga mageuzi yoyote kwa tume hiyo, ikisema kuna hatari ya vyama vya kisiasa kuingilia uhuru wake.

“IEBC inapaswa kufanyiwa mageuzi miaka miwili baada ya uchaguzi mkuu kukamilika ili kuepusha hali ambapo maafisa wake wakuu wanaingiliwa na wanasiasa mara tu baada ya uchaguzi,” akasema Bw Wahome.

Makundi mengine yaliyowasilisha maoni yao Ijumaa ni kundi la Youth for BBI na Kamati Maalum ya Kusimamia Vyama vya Kisiasa.