Makala

RIZIKI: Amejiimarisha kibiashara licha ya magumu 

February 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WANGARI Igoto anapoiamkia gange yake alfajiri na mapema kila siku ana kila sababu ya kutabasamu na kumshukuru Mungu.

Akiwa mkazi wa Murera, Ruiru, ni muuzaji wa matunda tofauti kijumla katika soko la Marikiti, lililoko jijini Nairobi.

Akivuta mawazo yake nyuma, anaona taswira ya mengi mazito na magumu aliyopitia kutika kusukuma gurudumu la maisha. Ni mama wa watoto wawili, mwanambee yaani kifungua mimba, mwenye umri wa mika 21, na ambaye yuko chuo kikuu na yule mdogo, 4.

Mama huyo anasema alijifungua kitinda mimba akiwa kidato cha tatu, na hakuwa na budi ila kusitisha masomo kwa muda wa mwaka mmoja ili kuitika majukumu ya uzazi.

“Nilikuwa na kiu cha elimu, na mwaka mmoja baadaye nikarejea shuleni,” anaiambia ‘Taifa Leo’.

Hatimaye, alifanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, na kulingana na simulizi yake hakuweza kuendeleza azma yake kupata elimu kwa kile anataja kama ukosefu wa karo.

“Baba alifariki tukiwa wachanga hivyo basi mama alikuwa ‘singo matha’, nililazimika kuruhusu wazawa wenza wadogo nao wafikie nilipofika,” anafafanua.

Wangari, 40, anasema alifanya vibarua vya hapa na pale, angaa kuweza kukimu mwanawe ambapo alichukua nafasi ya kuwa mama na baba.

“Sikubagua kazi, kuanzia shughuli za ujenzi, kulimia watu mashamba hadi dobi,” aelezea.

Ni katika harakati hizo alikutana na mwanamume ambaye aliishia kuwa mchumba wake, kilele kikawa kufunga pingu za maisha. Kwa udi na uvumba, Wangari anaeleza kwamba alihitaji ndoa na alifanya kila awezalo kuhitimisha majukumu kama mke na mama.

Ni katika ndoa hiyo mama huyo alijaaliwa mtoto wa pili, huo ukiwa mwaka wa 2015. Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye, anaeleza kwa masikitiko kwamba mume wake aliaga dunia baada ya kuugua Saratani.

Mauti ya mumewe, lilikuwa pigo kuu ikizingatiwa kuwa alifariki wakati alipomhitaji kwa hali na mali. Katika familia na maboma mengi, mume anapoondoka si wajane wengi wanaosalia kwa sababu ya unyanyapaa. Mashemeji wananyooshewa kidole cha lawama kwa ubaguzi huo.

Wangari anasema lililoanza kama mzaha kurushiwa maneno ya kejeli, liliishia kufurushwa katika boma alilooleka. “Niliondoka na wanangu bila chochote,” asema.

Kulingana na Dianah Kamande, mwasisi wa shirika la Come Together Widows and Orphans Organization, ambalo hutetea maslahi ya wajane na mayatima, kiini hasa cha masaibu ya aina hiyo ni urithi wa mali aliyoacha mume.

“Kuna wanaopitia unyama wakifukuzwa na ni jambo la kuhuzunisha. Ni muhimu familia itambue wazi kuwa mjane ni mmoja wao na sote tunaishi kwa mapenzi ya Mungu,” Dianah anasema.

Endapo changamoto hizo zinavuka mipaka, mdau huyo hata hivyo anahimiza mwathiriwa kuondoka mara moja. Pia anashauri umuhimu wa kujiunga na mashirika yanayoangazia unyanyapaa miongoni mwa wajane na mayatima.

“Mengi ya mashirika hayo hutetea haki zao na hata kuwapiga jeki kujiimarisha kimaisha,” aeleza.

Hata ingawa kuanzisha awamu nyingine ya maisha ilikuwa hatua ngumu, Igoto Wangari anasema alifanikiwa kuwekeza katika biashara ya matunda kupitia usaidizi wa bintiamu yake. Huyauza kijumla, ambapo hutegemea mawakala wanaoyatoa mashambani kwa wakulima.

Mjasirimali huyo anasema katika ruwaza yake ya miaka kumi ijayo, anapania kuanzisha kiwanda cha uongezaji thamani kwa matunda.

Hilo anamaanisha, kuunda bidhaa zitokanazo na matunda kama vile juisi au sharubati na pia kuyakausha ili kudumu muda mrefu.