• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
DOMO KAYA: Mungu akulaze pema

DOMO KAYA: Mungu akulaze pema

Na MWANAMIPASHO

MAZISHI yake Rais wa pili wa taifa hili Hayati Daniel Toroitich Arap Moi yalikamilika rasmi Jumatano ambapo alilazwa nyumbani kwake Kabarak, Nakuru.

Maombolezo ya Moi yalidumu kwa zaidi ya wiki. Kila Mkenya alifuatilia sababu hata kama hungelikuwa na nia hiyo, bado ungelazimika tu. Kila stesheni iwe runinga au redio au magazetini, stori zote zilimhusu Mzee Moi.

Mzee Moi alitawala taifa hili kwa miaka 24 kabla ya kuacha uongozi. Wakubwa wetu wanatuambia hafla ya mazishi yake ilikuwa kubwa hata zaidi ya mtangulizi wake hayati mzee Jomo Kenyatta. Laiti angelikuwa hai kushuhudia mapambo na mbwembwe zilizoandama mazishi yake, hata yeye mwenyewe angeshangaa. Naweza kusema ilikuwa bonge la pati.

Wakati haya yakijiri, ilitokea msiba mwingine kwenye tasnia ya Showbiz hapa nchini. Msiba huu ulimhusu msanii wa injili Papa Dennis. Mpaka sasa kifo cha Papa Dennis hakijanikaa sawa akilini.

Kifo chake kilitokea usiku wa Ijumaa iliyopita ambapo anaripotiwa kujirusha kutoka ghorofa ya saba katika jengo moja mjini Nairobi na kufariki papo hapo. Chanzo cha kifo chake kinasemekana kuwa msongo wa mawazo.

Nilipozipokea taarifa za kifo cha Papa Dennis, sikuamini. Nilikuwa kwenye Instagram nikipitia kutaka kujua nani kani-follow au nani kani-unfollow. Mara nikafika kwa posti yake Weezdom na kuikuta picha yake Papa iliyoandamanishwa na rambirambi. Mara moja nikampigia simu na akanipasha.

Nakumbuka nikiketi kitandani na machozi yakanitiririka. Nilihisi uchungu ambao ulinikumbukisha kifo cha mdogo wangu Daniel Mwangi aliyeniacha zamani kidogo katika mazingira ya kutatanisha. Kifo cha Papa kilinirudisha kule. Bado sijaweza kuamini vipi Papa aliamua kujitoa uhai. Sikutegemea.

Kilichoniliza ni hichi. Katika miaka saba ya uandishi wa showbiz, sijawahi kukutana na msanii mwenye hulka ya kujali kama yake Papa. Kwa kawaida hawa mastaa wetu bwana huringa sana, hujiona kuwa levo nyingine kama sio sayari tofauti na wewe. Hata kukuamkua tu inakuwa ishu. Toka nilipomfahamu Papa, jomba alifanya tabia ya kunijulia hali mara kwa mara. Angenipigia simu tu kunisalimu na kutaka kujua naendelea vipi?

Wakati mwingi msanii anapokupigia simu hasa kama wewe ni mwandishi wa burudani, aghalabu huwa anataka kitu kutoka kwako. Sikuona hiki kwa Papa. Angenipigia simu kunipa salamu, au kunialika tushiriki kombe la kahawa. Alinikutanisha na wadau mbalimbali wa sanaa na kuifanya netiwaki yangu kuzidi kunawiri. Nilipokuwa nagombea tuzo fulani, niliona alivyokuwa akihangaika kunipa sapoti kwa kuwaomba mashabiki wake wanipigie kura. Nina usahibu na maceleb kadhaa, ila mahusiano yetu hayajawahi kufika hapa.

Sasa kaondoka Papa sijui ni celeb yupi atakuwa akinipigia simu japo kutaka kunijulia hali. Sio kwa maringo yao. Nimeshindwa kufuatilia kiini cha kifo cha Papa ila naambiwa tangu alipotemwa na meneja wake wa zamani Sadat Muhindi Machiu 2019, ndipo mambo yalianza kumwendea kombo. Ghafla akasota, akakosa hela, yale maisha ya anasa aliyokuwa nayo yakapotea. Pamoja na maisha yale, watu wengi hawakuelewa kwamba ni Sadat ndiye alikuwa akimgharimia. Sijui mkataba wao ulikuwa wa aina gani ila nafsi yangu inanifanya kuamini kwamba Papa alitumiwa sana bila ya kupata faida

Sijui ilipolala nafsi yake leo ila natumai ni panapolazwa wengine wema. Papa kaondoka na kuniacha na majuto makubwa sana. Najuta ni kwa nini nilichukulia kuwa kitu cha kawaida kitendo chake cha kuishi akinijulia hali. Hili daima litaishi kunitesa. Papa Dennis mdogo wangu, nenda kwa amani tutaonana baadaye.

You can share this post!

ANA KWA ANA: Amerejea kwa fujo!

Mkandarasi wa ujenzi barabara ya Lamu-Garsen asitisha...

adminleo