• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Watoto wawili wapatikana katika shimo la choo Juja wakiwa wameuawa

Watoto wawili wapatikana katika shimo la choo Juja wakiwa wameuawa

Na LAWRENCE ONGARO

WATOTO wawili wamepatikana katika shimo la choo wakiwa wameuawa katika kijiji cha Riuriro, Murera mjini Juja.

Nyanya ya watoto hao wawili alikuwa amepiga ripoti kituo cha polisi cha Ruiru baada ya kupata habari za kifo chao na kushuhudia miili yao ilipotolewa kwenye shimo hilo.

Imeelezwa kwamba mkazi mmoja wa eneo hilo aliwaona watoto hao wawili wakiandamana na mtu fulani ambaye hakuweza kutambuliwa na baada ya siku moja, miili yao ilipatikana kwenye shimo hilo.

Kulingana na ripoti za polisi ni kwamba mshukiwa huyo alikuwa mume wa mama ya mmoja wa watoto hao na baada ya kukosana walikorofishana na kuachana.

Hata hivyo, mama huyo aliwaacha watoto hao na nyanya yao huku akisafiri nchini Italia kwa shughuli za kikazi.

Watoto hao ambao waliachwa na nyanya yao ni Linus Macharia (7), na Prince Muchina (6), ambao waliripotiwa kupotea baada ya kukosa kurejea nyumbani kutoka shuleni.

Nyanya wa watoto hao Joyce Wangechi alisema alisema yeye ndiye mlezi wa watoto hao baada ya mama huyo kwenda ng’ambo kwa shughuli za kikazi.

Miili hiyo ilitolewa katika shimo hilo walipatikana na majeraha mabaya sana ya visu huku miili hizo zikionekana kuharibika.

“Mimi nilipata habari kuhusu mauaji hayo kutoka kwa wakazi wa hapa baada ya kusema ya kwamba miili miwili ilionekana imetupwa katika lindi la choo,” alisema Bi Wangechi.

Alizidi kuelezea polisi ya kwamba mshukiwa alikuwa mtu wa fujo nyingi kwa muda wa miezi kadha walipokuwa pamoja – na mwanamke aliyesafiri ng’ambo – kama wachumba.

“Alikuwa akimpiga ovyo bila sababu. Hata kuna wakati nilitaka aachane naye ili apate amani,” alisema Bi Wangechi, nyanya ya watoto hao.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Juja Bi Dorothy Migarisha, tayari wamemshika mshukiwa wa mauaji hayo na anaendelea kuzuiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani ili afanyiwe mashtaka.

“Tutaendelea kumzuilia mshukiwa huyo kwa siku chache ili tujue ukweli wa mambo kabla ya kumwasilisha mahakamani ashtakiwe,” akasema Bi Migarisha.

Kwa wakati huu mshukiwa amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Juja huku akiendelea kuhojiwa zaidi kuhusiana na mauaji hayo ya watoto hao.

Miili ya wawili hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha General Kago mjini Thika, huku familia ikingoja kupata ripoti kamili kuhusu mauaji hayo.

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Ole wenu mnaotegemea nguvu za mikwanja...

Afungwa jela miaka miwili kwa kupatikana akimiliki nyoka

adminleo