Makala

KINAYA: Tumempumzisha Mzee, sasa turudieni unafiki wetu tusioonea haya kuuishi

February 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

KUONDOKEWA kubaya.

Naam, si raha kufiwa na mtu uliyempenda. Hata usiyempenda. Sikumbuki hata siku moja nikisikia mfu akikaripiwa mazishini.

Kisa na maana? Mwafrika hamsemi aliyetangulia mbele ya haki eti. Lakini binafsi sidhani ni suala la heshima, La hasha! Nakisia ni hofu ya kumsema mtu akutokee kwenye ndoto.

Hata mimi singetaka kupata mazingaombwe. Hebu tafakari mwendazake Mzee Kirungu tuliyemwogopa ajabu kwa miaka 24 akikutokea usiku wa kiza kwenye ndoto.

Hebu tafakari akikuuliza, huku kakunyooshea kirungu kama kwamba anataka kukivunjia kichwani pako: ‘Wewe mtu wa fitina na siasa mbaya, ulinisemaje mazishini yangu?’

Hapo, sikufichi, ndipo unaamka mwingi wa fujo, huku ukipiga nduru na kutoroka tuputupu ikiwa hukuvaa chochote ukilala! Mwoga zaidi ataamka kisha azimie na kukata roho!

Mzee Kirungu, akiwa hai na mautini, aliogofya ajabu. Wewe umesikia wangapi wakimsema vibaya wakati wa mazishi? Mzee ameunganisha nchi hata kwenye mauti.

Ni majinuni mmoja tu mpayukaji, ambaye nakumbuka akimpayukia Baba Jimmy hivyo nayachukulia mazoea, aliyethubutu kupanua kinywa wakati wa ibada ya wafu Nairobi.

Alibebwa juujuu, huku kinywa kazibwa kwa maganja ninayoshuku yakinuka majasho na mtutu wa bunduki, akasombwa mbali tusikojua!

Enzi za Baba Jimmy alipopayuka mwehu wa watu huyo na kutwaliwa vilevile, aliibuka baada ya siku tatu akanijia ofisini na kuniambia niripoti kwamba kafinywa sehemu nyeti.

Sasa mara hii sijui wafinyao walifinya nini kwa maana wataalamu wananiambia zikifinywa mara moja huwa basi, jongoo hapandi mtungi milele!

Turejee waliko wanasiasa. Lazima nikusafie nia, nikwambie sikufurahishwa sana na amani, umoja na ushirikiano tulioona kati ya wanasiasa wakati wa msiba huo wa juzi.

Bila shaka napenda amani; ina tija zaidi kuliko kelele. Amani ikiwepo ninaamini kwamba wakora tuliochagua wamebadilika, wawi wakawa wema, hivyo tusubiri matunda.

Hata hivyo, ninajua kinyume cha imani yangu hiyo kina uhalisia zaidi. Wanapoungana wanasiasa wetu, ingia hofu mara moja!

Nyakati zote ambapo wanasiasa wa upinzani na serikali wameungana, Mkenya ametokea kuumizwa kwa jinsi isiyorekebika.

Waliwahi kuungana wakajiongezea mishahara, wakaungana wakala hongo na kukataa kupitisha hoja ya kutokuwa na imani na wahujumu uchumi.

Je, unakumbuka ile kashfa ya sukari iliyokuwa na almasi ambayo iliibuka yapata miaka miwili iliyopita hivi?

Wakati huo waliungana, wakaingia vyooni kimyakimya, wakapokea hongo hata ya Sh10,000, kashfa ikafa hivyo.

Hapo labda tuwaelewe tu, tuwatolee kisingizio kwamba msalani kunahitajika adabu, tena hakunukii, kunanukia.

Ukitaka waongee wakiwa huko, wawekee marashi. Lakini nakuhakikishia watakinywa tu ikiwa hutaondoa hongo.

Amini usiamini, hili ni ombi langu kwa wanasiasa wetu kwamba kwa vile tumempumzisha Mzee Kirungu, warejee uwanjan I kwa fujo na kukabana makoo kuhuru BBI.

Maisha hayatamanishi watu wanapoigiza amani. Hayo ni maisha bandia. Kenya tunataka uhalisia, watu wararuliane magwanda, wengine waketishwe mavumbini, walielie kitoto!

Si kwamba napenda ghasia. Nielewe: uzoefu wangu unanionyesha kwamba Kenya hupiga hatua muhimu tunapokuwa na maoni kinzani, tukatafuta mapatano baada ya kukwaruzana.

Amani kamwe haipatikani ila kwa ncha ya upanga. Ukiwaona waambie waondoke kwenye jukwaa la msiba, wapande la BBI, tukutane mashinani.

 

[email protected]