• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
MWANASIASA NGANGARI: Mwanadiplomasia nguli aliyeuawa kinyama 1990

MWANASIASA NGANGARI: Mwanadiplomasia nguli aliyeuawa kinyama 1990

Na KEYB

ROBERT John Ouko ambaye zamani alihudumu kama Mbunge wa Kisumu Mjini, atakumbukwa kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini ambaye alikuwa mwanadiplomasia shupavu, lakini aliyeuawa kinyama mwezi kama huu mnamo 1990.

Alishikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka sita chini ya utawala wa rais wa zamani hayati Daniel Arap Moi; kati ya miaka ya 1979 na 1983 na tena kati ya mwaka wa 1988 hadi 1990. Hizo ni nyakati ambapo taifa hili lilikuwa likipitia wakati mgumu haswa kiuchumi.

Isitoshe, ni wakati ambapo utawala wa KANU ulikabiliwa na presha nyingi kutoka ndani na nje kutokana na rekodi yake mbaya ya uvunjaji wa haki za kibinadamu na uendelezaji wa ufisadi.

Lakini Ouko aliutetea utawala wa Moi ndani ya nchini na kimataifa, kwa bidii na weledi wa kupigiwa mfano, licha ya shutuma nyingi kutoka kwa viongozi wa kidini, makundi ya wanaharakati kama vile Mwakenya. Serikali hiyo pia ilielekezewa lawama nyingi na viongozi wa siasa za upinzani, mabalozi wa mataifa ya kigeni na mashirika ya kimaendeleo kama vile Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia.

SHUTUMA

Kwa mfano, Ouko aliwaacha wengi vinywa wazi kuhusu jinsi alivyoitetea Kenya, dhidi ya shutuma hizo, katika mkutano wa mawaziri wa masuala ya kigeni wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika jijini Oslo, nchini Uswidi mnamo mwaka wa 1989.

Na mnamo Januari 1990 wakati wa Hafla ya Maombi nchini Amerika, sifa za Rais Moi na utawala wake, zilisemekana kuimarika kwa kiwango fulani, kutokana na kazi nzuri ambayo Ouko alifanya katika nyanja za kimataifa.

Rais Moi alihudhuria mkutano huo akiandamana na Ouko, aliyekuwa Waziri wa Viwanda marehemu Nicholas Biwott pamoja na maafisa wengine wa serikali.

Ouko alizaliwa katika kijiji cha Nyahera mnamo mwaka wa 1932. Alisomea Shule ya Msingi ya Ogada na ile ya Upili ya Nyang’ori kabla ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Siriba, Maseno. Baadaye, aliwafanyakazi kama mwalimu wa shule ya msingi. Aligura kazi hiyo baada ya miaka mitatu na akaajiriwa kama Afisa wa Ukusanyaji Mapato katika Wilaya ya Kisii (sasa kaunti ya Kisii).

Mnamo 1958, ndoto yake ya kujiendeleza kielimu ilitimia alipofaulu kujiunga na Chuo Kikuu cha Haile Selassie jijini Addis Ababa, Ethiopia. Alihitimu mnamo 1962 kwa kupata shahada ya kwanza katika taaluma ya Utawala, Uchumi na Sayansi ya Kisiasa.

Aliendelea kukwea ngazi ya masomo na akatua katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambako alisomea shahada ya Diploma katika taalamu ya Diplomasia na Mahusiano na Kimataifa.

Kenya ilipopata uhuru wake mnamo 1963 Ouko aliajiri kama Naibu Katibu katika afisi ya Gavana na hapo ndipo ujuzi wake ulitambuliwa. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Katibu (PS) katika wizara ya Ujenzi na kisha akahamishwa hadi wizara ya Mashauri ya Kigeni baada ya mwaka mmoja.

Akihudumu kama Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni aliweza kuteuliwa kama Mwenyekiti wa Baraza Tawala la Shirika la Leba Ulimwenguni (ILO).

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilipobuniwa mnamo 1969, Ouko aliteuliwa kuwa Waziri wake wa Fedha na Usimamizi. Nyota yake iling’aa hadi akapewa shahada ya heshima ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Pacific Lutheran jimboni Seattle nchini Amerika mnamo 1971.

Lakini jumuiya ya EAC iliposambaratika mnamo 1977, Dkt Ouko alirejeshwa nyumbani na kuteuliwa na Rais Jomo Kenyatta kuwa mbunge maalum na baadaye akateuliwa kuwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi.

Rais mstaafu marehemu Moi ambaye aliingia usukani baada ya Mzee Kenyatta kufariki mnamo Agosti 1978, alimdumisha Dkt Ouko katika baraza lake la mawaziri kwa misingi ya tajriba aliyopata akihudumu kama Waziri wa Jumuiya ya EAC.

Kufikia wakati huo, hamu ya kujitosa katika siasa ya uchaguzi ilikuwa imemfika na ndiposa mnamo 1979 akawania na kushinda kiti cha ubunge cha Kisumu Mashambani. Na alitetea kiti hicho katika uchaguzi mkuu uliofuata mnamo 1983 na akaibuka mshindi.

Lakini baada ya siasa za Kisumu kuwa zenye ushindani mkubwa, Dkt Ouko alibadili eneo bunge na kuhamia eneo bunge la Kisumu Mjini katika uchaguzi mkuu wa 1988 na akashinda. Ni akihudumu kama mwakilishi wa eneo bunge hilo bungeni ambapo Rais Moi aliweza kumteua kuwa waziri katika wizara za Leba, Mipango na Maendeleo ya Kitaifa, Viwanda na Mashauri ya Nchi za Kigeni.

Mnamo Januari 27, 1990, Dkt Ouko alikuwa mmoja ya mawaziri walioandamana na Rais Moi katika Hafla ya kila Mwaka ya Maombi jijini Washington, Amerika. Ujumbe huo wa Kenya ulirejea nyumbani mnamo Februari 4. Na mnamo Februari 13 Dkt Ouko aliuawa na mwili wake ukatupwa katika msitu mmoja karibu na eneo la Got Alila. Sehemu ya mwili huo ulikuwa umechomwa kwa tindikali.

UCHUNGUZI

Baadaye serikali ilianzisha uchunguzi kuhusu chimbuko la kifo cha Dkt Ouko kwa kualika wapelelezi wa Scotland Yard, Nchini Uingereza, wakiongozwa na John Troon.

Rais Moi alikana madai kuwa serikali yake ilihusika katika mauaji akimtaja Ouko kama “rafiki na mshirika mkubwa”. Aliahidi kuwa serikali yake ingefanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa wale waliomuua Ouko wamekamatwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Wapelelezi hao waliwataja aliyekuwa Waziri wa Viwanda Nicholas Biwott, aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Hezekiah Oyugi na alikyeuwa Mkuu wa Mkoa wa Nakuru Jonah Anguka kama washukiwa wakuu wa mauaji hayo. Mbw Biwott na Oyugi walikamatwa na polisi lakini wakaachiliwa baadaye kwa madai kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuwahusisha na “mauaji ya Dkt Robert Ouko.”

Naye Bw Anguka alitorokea Amerika ambako aliishi kwa zaidi ya miaka 10 kuwepa kukamatwa.

Lakini mwaka mmoja baada ya mauaji ya Ouko ilifichuka kuwa akiwa Amerika pamoja na Rais Moi, waziri huyo alifanya mashauriano na Rais wa Amerika wakati huo George Bush katika Ikulu ya White House.

Inasemekana kuwa Rais Moi hakuwa na habari kuhusu mkutano kati ya Ouko na Rais Bush jambo ambalo lilimkasirisha zaidi “waziri mmoja ambaye alikuwa katika ujumbe wa Rais Moi.”

Hata hivyo, mamlaka nchini Amerika ilipuuzilia madai kuwa Dkt Ouko alikutana na Rais Bush.

Lakini mnamo mwaka wa 2017, wakati wa maadhimisho miaka 25 baada ya mauaji ya Dkt Ouko, mjane wake Christabel Ouko, alithibitisha kuwa mumewe alikutana na Bush. Alisema balozi wa Amerika nchini Kenya wakati huo Smith Hempstone alimtumia picha ya mkutano huo kati ya Ouko na Bush.

Kufikia sasa kitendawili kuhusu mauaji ya Dkt Ouko, sawa na mauaji ya watu wengine mashuhuri miaka ya nyuma, hakijateguliwa.

You can share this post!

KINAYA: Tumempumzisha Mzee, sasa turudieni unafiki wetu...

Nguli wa Kiswahili wamzuru manju stadi Maulidi Juma

adminleo