• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Mutahi Kagwe, Maina na wengine sita kupigwa msasa na bunge

Mutahi Kagwe, Maina na wengine sita kupigwa msasa na bunge

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Seneta wa Kaunti ya Nyeri Mutahi Kagwe na Betty Maina; watu ambao waliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa nyadhifa za Mawaziri wa Afya na Ustawi wa Kiviwanda mtawalia watapigwa msasa na bunge juma lijalo.

Hii ni kulingana na notisi iliyochapishwa na Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai mnamo Jumamosi ambapo alitangaza kuwa wawili hao watafika mbele ya kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi mnamo Alhamisi.

Bw Mutahi aliteuliwa kwa mara nyingine katika baraza la mawaziri mwezi Januari Rais alipotekeleza mabadiliko serikalini ambapo alimpiga kalamu Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na Waziri wa Biashara Peter Munya akahamishiwa wizara hiyo.

Naye Waziri wa Afya anayeondoka Sicily Kariuki alihamishwa hadi Wizara ya Maji.

Katika kikao cha kamati hiyo ambacho kitaongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Bw Kagwe na Bi Maina watajibu maswali kutoka kwa wabunge huku wakijaribu kuwashawishi kuhusu ufaafu wao kwa nyadhifa hizo.

Bw Sialai pia alisema watu sita ambao Rais Kenyatta aliwateua kushikilia nyadhifa za Katibu wa Wizara pia watapigwa msasa na kamati zinazohusika na wizara watakazohudumia.

Wao ni Johnson Weru, Dkt Jwan Ouma, Mary Kimonye, Balozi Simon Nabukwesi, Solomon Kitungu na Enock Momanyi, ambao waliteuliwa kuhudumu katika wizara za Biashara, Mafunzo ya Kiufundi, Utumishi wa Umma, Elimu ya Vyuo Vikuu, Uchukuzi na Mipango ya Miji, mtawalia.

Wakiidhinishwa na wabunge, Mutahi, Maina na watu hao sita walioteuliwa Makatibu wa Wizara watateuliwa rasmi na Rais Kenyatta na kuanza kutekeleza majukumu yao.

You can share this post!

Mikutano ya BBI kuisha Machi – Raila

Orengo ataka Dkt Ruto atoe maelezo kuhusu sakata...

adminleo