• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Polisi ndani baada ya washukiwa kuhepa

Polisi ndani baada ya washukiwa kuhepa

Na GEORGE MUNENE

AFISA wa polisi amekamatwa katika Kaunti ya Kirinyaga kuhusiana na kisa cha washukiwa wanne kutoweka kizuizini mwa polisi katika hali ya kutatanisha.

Afisa huyo wa polisi alikamatwa mnamo Jumamosi kwa tuhuma za kuwasaidia washukiwa hao Martin Ndung’u, Willis Githuku, Charles Mwangi na Martin Ndung’u kutoroka kutoka Kituo cha Polisi cha Sagana.

Kulingana na Kamanda wa Polisi eneo la Mwea Magharibi Abdilahi Adan Alio afisa huyo aliondoka wakati wa zamu yake Ijumaa wiki iliyopita katika hali ambayo haikueleweka.

“Afisa huyo aliondoka na kuacha kituo chake bila mlinzi. Baadaye alidai alienda hospitalini baada ya kuugua. Alirejea saa tatu asubuhi mnamo Jumamosi,” alisema Bw Alio.

Uchunguzi wa polisi unaeleza kuwa afisa huyo aliondoka katika kituo kwa nia ya kuwapa washukiwa hao nafasi ya kutoroka seli.

Washukiwa hao wanaodaiwa kuwa majambazi sugu wa wizi wa mabavu walitazamiwa kufikishwa katika Mahakama ya Baricho kuhusiana na misururu ya wizi katika maduka ya Mpesa kaunti za Kirinyaga na Murang’a.

Mbunge wa Mwea Kabinga Wathayu, alisema kisa hicho kilishangaza sana na kimefanya wakazi waishi kwa hofu kubwa kwani washukiwa waliotoroka walikamatwa kwa madai ya kuwa wezi sugu.

Mbunge huyo ambaye ni mwanachama wa kamati ya bunge kuhusu usalama, alishangaa jinsi washukiwa walio chini ya ulinzi wa polisi kwa saa 24 kila siku waliweza kutoroka.

Alitaka uchunguzi wa kina ufanywe ili yeyote aliyehusika kuwasaidia kutoroka aadhibiwe ipasavyo.

Washukiwa hao waliripotiwa kukata vyuma vya dirisha ya seli walimokuwa wamezuiliwa ndiposa wakatoroka.

Maafisa wa upelelezi waliokuwa wakiendesha kesi hiyo walikuwa wameomba korti kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 14 ili kuruhusu upande wa mashtaka kukusanya ushahidi zaidi.

Washukiwa hao bado hawajulikani waliko kufikia sasa, lakini polisi wamesisitiza kuwa wangali wanawasaka.

  • Tags

You can share this post!

Asilimia 92 ya maji ya Ziwa Victoria ni kinyesi na sumu!

Kanisa la ACK kupokea sadaka kwa M-Pesa kuzima ufisadi

adminleo