• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Msichana ‘aliyefufuka’ avutia umati

Msichana ‘aliyefufuka’ avutia umati

Na SHARON ACHIENG’

KWA wiki kadhaa sasa, wakazi wamekuwa wakimiminika katika kijiji cha Kiabonyoru, eneobunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira kujionea maajabu ya msichana aliyerudi nyumbani ilhali alikuwa ‘amezikwa’ mwaka uliopita.

Msichana Jackline Bosibori (sio jina lake halisi), ambaye ni yatima alikuwa akiishi na mjomba yake, aliponajisiwa na kutiwa mimba na wanaume wasiojulikana alipokuwa njiani kwenda kununua bidhaa dukani jioni mnamo 2018 alipokuwa na umri wa miaka 13.

Kukwepa ghadhabu za walezi wake, Bosibori aliamua kutoroka nyumbani.

Licha ya kuwa Bosibori ambaye sasa ana umri wa miaka 15, alirejea nyumbani (kwa mjomba yake) mnamo Januari 16, mwaka huu kutoka ‘mafichoni’ baada na kupata ‘kaburi lake’, wanakijiji bado hujazana bomani kwao kumwona.

Jamaa zake ‘walimzika’ miezi minane baada ya kutoweka walipotambua maiti iliyokuwa imeharibika kwenye mochari kijijini Eng’enta, kilichoko kilomita kadhaa kutoka mahali alipokuwa akiishi na mjomba yake.

Wanakijiji na jamaa wamekuwa wakimiminika nyumbani kwao katika kijiji cha Kiabonyoru, eneobunge la Borabu kuja kuona ‘mtu aliyefufuka’ ambaye sasa ni mama ya mtoto wa kike.

Aliambia Taifa Leo kuwa aliamua kutoroka nyumbani kutokana na aibu ya kuwa mama huku akiwa chini ya umri wa miaka 18.

“Nilihisi aibu kuendelea kuishi nyumbani huku nikiwa mjamzito. Niliamua kutoroka na nirejee baada ya kujifungua,” akaendelea huku akitokwa na machozi.

Bosibori alisema kuwa alikuwa na Sh4,000 alizotumia kusafiri kutoka Kaunti ya Nyamira hadi Siaya.

Alipofika Siaya mnamo Januari 11, 2019, alikutana na mwanamke aliyeamua kuishi naye baada ya kumsimulia masaibu yake.

“Alikubali kuishi nami hadi nijifungue. Nimekuwa nikiishi naye hadi sasa nilipoamua kurejea nyumbani,”akasema.

Alishutumu familia yake kwa ‘kumzika’ akiwa hai.

Hata hivyo, alisema kuwa amesamehe jamaa zake kwa kuzika mwili wa mtu mwingine wakidhani ni yeye.

Alisema kuwa sasa anataka kurejea shuleni na kuendelea na masomo yake ili kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari katika siku za usoni.

Kwa upande wake, mjomba yake alisema kuwa alifurahishwa na kurejea kwa mpwa wake ambaye walimzika zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

“Baada ya juhudi za kumtafuta kugonga mwamba tuliamua kwenda katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Nyamira. Jamaa na majirani waliokuwepo ‘walitambua’ moja ya maiti kwamba alikuwa Bosibori,” akasema mjomba yake ambaye jina lake limebanwa ili kulinda mwathiriwa wa unajisi.

Alisema, alikataa kuchukua maiti hiyo lakini familia ikasisitiza kwamba alikuwa Bosibori.

“Bosibori ni mrefu na mwembamba. Lakini maiti tuliyozika ilikuwa ya msichana mnene na mfupi. Baadhi ya wanafamilia walisisitiza kuwa maiti hiyo ilikuwa yake kuichukua na kwenda kuzika katika eneo la Mugirango Kusini mnamo Oktoba 2019,” akaelezea.

Mjomba wa Bosibori alisema kuwa hakuhudhuria na wala hakushirikishwa katika mipango ya mazishi hayo.

Alishikilia kuwa Bosibori hakuwa amekufa na huenda angerejea nyumbani siku moja.

Kulingana na Bw Japheth Mesa, ambaye ni jirani, maiti iliyozikwa kimakosa inafaa kufukuliwa na jiwe lizikwe kwenye kaburi hilo kwa mujibu wa mila na desturi jamii ya Abagusii.

Kamanda wa Polisi wa Nyamira Kaskazini Patrick Ngeiywa alisema kuwa wameanzisha uchunguzi kubaini ikiwa utaratibu wa sheria ulifuatwa kabla ya familia kuruhusiwa ‘kuzika’ mwili wa Bosibori.

You can share this post!

Maimamu waapa kujiunga na maandamano ya kupinga SGR

Rungu la Moi halitamtikisa Ruto Rift Valley – Mbunge

adminleo