• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Sportpesa watemwa EPL na klabu ya Everton

Sportpesa watemwa EPL na klabu ya Everton

Na GEOFFREY ANENE

WADHAMINI wa zamani wa Gor Mahia, AFC Leopards pamoja na Ligi Kuu ya Kenya (KPL), SportPesa wamepata pigo jingine baada ya klabu ya Everton nchini Uingereza kutema kampuni hiyo ya kamari.

SportPesa ilikatiza udhamini wake wote nchini Kenya mnamo Julai 2019 baada ya serikali kuwekea kampuni za kamari sheria kali.

Iikuwa ikifadhili Everton, inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kwa karibu Sh1.3 bilioni kila mwaka kuambatana na mkataba wa 2017.

Kampuni hiyo iliyoanzishwa 2014 inamilikiwa na watu kutoka Kenya, Bulgaria na Marekani.

Ilikuwa ikidhamini Shirikisho la Raga nchini (KRU) kwa Sh607 milioni, KPL kwa Sh450 milioni, klabu za soka za Gor (Sh325 milioni) na Leopards (Sh225 milioni), pamoja na kombe la SportPesa kati ya klabu za Kenya na Tanzania, ambayo mshindi alipata fursa ya kukabiliana na Everton.

Washindi wa kombe la SportPesa mwaka 2017 na 2018, Gor Mahia walilimana na Everton jijini Dar es Salaam, Tanzania kabla kukutana tena uwanjani Goodison Park mjini Liverpool.

Mabingwa wa mwaka 2019, Kariobangi Sharks walialika timu hiyo ya Uingereza jijini Nairobi mwaka jana.

Katika taarifa Jumapili, Everton ilisema kuwa uhusiano kati yake na na SportPesa utakatizwa mwisho wa msimu huu wa 2019-2020.

Klabu hiyo ya EPL ilikuwa imesaini kandarasi kubwa ya miaka mitano na SportPesa mnamo Mei 2017 baada ya kandarasi yake ya shati na kampuni ya vinywaji ya Chang nchini Thailand kutamatika.

Katika tovuti ya Everton, taarifa ilieleza: “Ni uamuzi mgumu, lakini unatupatia nafasi ya kufanya mipango bora ya kibiashara. Tunashukuru SportPesa kwa kazi tuliyofanya pamoja. Ushirikiano wetu uliwezesha kikosi cha kwanza kuzuru Afrika mara mbili.

“Aidha, ulituwezesha kukuza umaarufu na uhusiano wetu barani Afrika,” msemaji huo aliongeza.

Kabla ya kuondoka soko la Kenya, SportPesa inasemekana ilikuwa ikiunda Sh201 bilioni kila mwaka kutokana na beti ambazo Wakenya walicheza.

Tangazo hilo ni muziki mtamu kwa mashabiki wa Everton ambao hawakufurahia klabu hiyo kushirikiana na kampuni ya kamari mwaka 2017, hasa kwa sababu ya tatizo kubwa la uchezaji wa kamari dunia nzima.

Katika Ligi Kuu ya Uingereza, Brighton & Hove Albion, Sheffield United na Southampton ndizo klabu zisizo na udhamini wowote kutoka kampuni za kamari.

Kabla ya kuondoka soko la Kenya, SportPesa inasemekana ilikuwa ikiunda Sh201 bilioni kila mwaka kutoka kwa Wakenya.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Amezidi kwa ngoma hata nikiugua hanipi...

Gor, AFC wajua wapinzani katika Betway 16-bora

adminleo