Moi aombe familia ya Matiba msamaha kwa mateso – Koigi Wamwere
NA PETER MBURU
MPIGANIAJI wa ukombozi wa pili Koigi Wa Wamwere Jumatatu alimtaka rais mstaafu Daniel Moi kuomba familia ya marehemu Kenneth Matiba msamaha kwa mateso aliyopitia ndani ya uongozi wake, huku wazee wa Bonde la Ufa wakiitaka serikali kumzika kishujaa kama alivyozikwa Nelson Mandela.
Bw Wamwere alisema kuwa kifo cha Bw Matiba kilitokana na shida za kiafya alizopata wakati alipofungwa bila hukumu, na mateso aliyokumbana nayo akiwa jela.
Mbunge huyo wa zamani wa Subukia alimtaka Mzee Moi kuwa shupavu na kuiomba msamaha wakati taifa likiomboleza kifo cha kiongozi huyo, akisema ujumbe wa rambirambi haungetosha.
Alimtaja Bw Matiba kuwa kiongozi aliyejitolea kupigania Kenya huku akiitaka serikali kukiri makosa ya uongozi wa mbeleni mbele ya umma kama namna ya kuonyesha kufurahia matunda aliyopigania marehemu Bw Matiba.
“Ninatarajia kuwa siku zijazo wakati taifa likiomboleza, mzee Moi atapata ushupavu wa kuomba familia ya Matiba msamaha, mbali na kutuma rambirambi kwani ni kutokana na kifungo alichopata wakati wa Moi na mateso yaliyofuata vilivyompa magonjwa ambayo alirudi nyumbani nayo na kufa baadaye,” Bw Wamwere akasema.
Kulingana na Bw Wamwere, mateso waliyopata viongozi waliofungwa bila kuhukumiwa yalikuwa mengi na machungu, yakiwemo kunyimwa matibabu na kutengwa kando na watu.
“Kutengwa kando na watu kwa saa 23 na nusu kila siku ni uchungu, ni kutengwa kikamilifu na hata unapougua haupewi huduma,” akakumbuka mbunge huyo wa zamani wa Subukia, ambaye pia aliwahi kufungwa kifungo sawa.
Kwa upande mwingine, wazee wa kutoka Bonde la Ufa wakiongozwa na mwenyekiti wao Gilbert Kabage waliitaka serikali kujitwika mzigo wa kumzika mzee Matiba, huku wakisisitiza kuwa marehemu anapasa kuzikwa kishujaaa kama alivyozikwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela.
“Kushikwa na kufungwa kwake ni baadhi ya mambo yaliyoudhi, lakini matunda yake tumeyaona kama taifa. Marehemu anafaa kuzikwa kishujaa kama Bw Mandela kwani pia naye alipigania Uhuru wa wakenya kutoka kwa wakenya wakoloni na matunda yake tunayaona,” akasema mzee Kabage.
“Mipango ya mazishi inafaa kuwa jukumu la serikali kama njia ya kukiri kuwa ilikosea kwa kumtesa, na kufurahia shujaa wa taifa letu,” Bw Kabage akasema.