• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Balozi wa Saudia lawamani kwa kuvuruga Supkem

Balozi wa Saudia lawamani kwa kuvuruga Supkem

 Na WACHIRA MWANGI

WANACHAMA wa Baraza Kuu la Waislamu (SUPKEM) tawi la Pwani wametoa wito kwa balozi wa Saudi Arabia hapa nchini Mohamed Khayat, akome kuingilia masuala ya uongozi wa baraza hilo kwa kupinga uongozi wa mwenyekiti wa sasa Hassan ole Naado.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Muungano wa Vijana Waislamu Khamis Juma Mwaguzo, wanachama wa Supkem kutoka Kwale, Likoni, Mvita Changamwe na Kisauni, walisema kwamba wameshangazwa na hatua ya Bw Khayat kuingilia uongozi wa Supkem.

“Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba hatuendi kinyume na katiba ya Supkem. Tunajua balozi huyo anaelekezwa visivyo na watu fulani wala hatutaruhusu mwenyekiti wetu Hassan Ole Naado aondolewe ilhali alichaguliwa kulingana na Katiba ya Supkem,” akasema Bw Mwaguzo akiwa katika msikiti wa Mbaruku mjini Mombasa.

Aliongeza, “Tunaheshimu sana Saudi Arabia kutokana na uhusiano mzuri kati yao na Kenya. Pia tunashukuru serikali yao kwa kuhakikisha kwamba ibada ya Hajj kila mwaka inaendelea bila tatizo lolote,” akaongeza.

Alisisitiza ushirikiano wa Kenya na Saudi Arabia ni imara na si vyema kwa Bw Khayat kutumia watu fulani kupendekeza uongozi mpya kwa Supkem au kuingilia mambo ya baraza lenyewe.

Alipofikiwa, Bw Ole Naado alikataa kuzungumzia suala hilo huku ikibainika aliandika barua ya malalamishi kwa ubalozi wa Saudia Arabia nchini.

“Mheshimiwa masuala ambayo yamechochea kuandikwa kwa barua hii yanahusiana na mwenendo wako wa kibinafsi. Umekuwa ukitumia mbinu za kichinichini kushinikiza kuondolewa kwa mwenyekiti wa sasa ili nafasi yake ichukuliwe na mtu unayempendekeza lakini hilo si suala la kimaadili,” ikasema barua hiyo.

Bw Khayat hata hivyo alijitetea dhidi ya kufahamu lolote kuhusu barua anayodaiwa kuandikia Supkem, akisema ubalozi huo haujawahi kuingilia masuala ya ndani ya Kenya au baraza hilo.

You can share this post!

Wataka waziri aagizwe kutoa mkataba wa SGR

Starlets waalikwa kuwania ubingwa wa soka ya wanawake...

adminleo