Wazazi wa wanafunzi waliofariki Kakamega hawajapokea pesa zilizochangwa kuwasaidia
Na CHARLES WASONGA
WAZAZI wa wanafunzi 15 wa Shule ya Kakamega waliofariki katika mkanyagano shuleni humo hawajapokea fedha zilikusanywa wakati wa ibada ya pamoja kuwaenzi wendazao siku 10 zilizopita.
Serikali ya kitaifa, vyama vya walimu na viongozi wa kidini walikusanya Sh5.3 milioni lakini baadhi ya wazazi wamelalamika kuwa hawajapokea mgao wao wa fedha hizo ilhali zilikusanywa kugharamia mazishi.
Kucheleweshwa kwa fedha hizo kumewaacha wazazi wa watoto hao kusaka fedha za mazishi kivyao.
Waathiri watatu wa mwisho wa mkasa huo walizikwa Jumamosi katika maeneo mbalimbali ya nchini.
Kila moja ya familia 14 zilitengewa Sh100,000 na Serikali ya Kitaifa, na Sh24,000 kati ya fedha hizo zilikatwa kugharamia ibada ya wafu. Mwathiriwa wa mwisho alifariki baada ya pesa hizo kutolewa.
Baraza la Magavana (CoG) lilichanga Sh2 milioni, Wizara ya Elimu (Sh1.4 milioni) na Hazina ya Serikali ya Kitaifa kuhusu Majanga –NGDF (Sh700,000) na chama cha KUPPET (Sh500,000).
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula walitoa Sh100,000 kila mmoja.
Lakini mnamo Jumanne Kamishna wa Kaunti ya Kakamega Pauline Dola alisema pesa hizo ziko salama. Alikuwa akijibu madai kwamba huenda pesa hizo zimetwaliwa na “baadhi ya maafisa wa utawala wa mkoa.”
“Sikuziweka pesa hizo katika akaunti yangu. Tunamsubiri gavana (Oparanya) aje wiki ijayo ili tuwaite wazazi na tuwape pesa zao,” akasema Bi Dola.
Aliongeza kuwa Bw Oparanya anasaka pesa zingine kwa ajili ya kuwafaa familia zilizopoteza wapendwa wao.
“Tuache kueneza uvumi usio na msingi,” Bi Dola akasema.
Naye Naibu Rais William Ruto alitembelea shule hiyo na kuahidi kwamba serikali itafidia familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika mkasa huo.
Wanafunzi hao walifariki mnamo Februari baada ya kunyagana shuleni mwao. Chanzo cha mkasa huo hakijabainika mpaka sasa.