Makala

GWIJI WA WIKI: Nderitu Wanjohi

February 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

MATUMIZI bora ya Kiswahili shuleni hutegemea sana kiwango cha ujuzi wa mwalimu, mtagusano alionao na wanafunzi na uelewa wake wa stadi za mawasiliano.

Siri ya kuwa mwalimu bora ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Huu ndio ushauri wa Bw Nderitu Wanjohi – mwalimu mstaafu wa Kiswahili na mpenzi kindakindaki wa gazeti la Taifa Leo ambaye kwa sasa ni mshirikishi wa mradi wa Newspapers in Education (NiE), mfugaji hodari na mfanyabiashara maarufu mjini Nyeri.

Maisha ya awali

Nderitu alizaliwa mnamo 1958 katika kijiji cha Ihururu, Kaunti ya Nyeri akiwa mwanambee katika familia ya wavulana sita wa marehemu Mwalimu Charles Wanjohi na Bi Salome Wambui. Hadi kufariki kwake, Bw Wanjohi alikuwa Afisa wa Elimu katika eneo la Subukia, Nakuru katika enzi za Wakoloni.

Baada ya kupata elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Ihururu kati ya 1965 na 1972, Nderitu alijiunga na Shule ya Upili ya St Mary’s Boys, Nyeri mnamo 1973 na akajipata katika darasa moja na Gavana wa sasa wa Kaunti ya Nyeri, Mheshimiwa Mutahi Kahiga.

Alisomea St Mary’s Boys kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Karima Boys, Nyeri alikofanyia mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Kidato cha Nne (KCE) mwishoni mwa 1976. Ingawa alizoa alama nzuri katika mtihani huo, alihiari kuwasaidia wazazi wake kufanya kazi mbalimbali za nyumbani na kujishughulisha sana na masuala ya kilimo.

Ilikuwa hadi 1979 alipopata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Shamata, Kaunti ya Nyandarua. Akiwa huko, alijisajili kwa masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’ mnamo 1978. Alifanya mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Kidato cha Sita (KACE) mwishoni mwa 1980 na akaendelea kuwa mwalimu shuleni Shamata kwa miaka mitatu zaidi.

Anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa walimu wake waliomshajiisha masomoni na kumwelekeza katika mkondo wa nidhamu kali. Bi Ngunju na marehemu Bi Kiretai ndio waliomtandikia zulia zuri la kukichapukia Kiswahili kwa ghera na idili shuleni Ihururu.

Waliopanda na kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya Nderitu ni Bw Njoroge Magoko, Bw Kamau Kagunda na Gichohi Waihiga ambao walikuwa wahadhiri wake katika Chuo cha Ualimu cha Kagumo, Kaunti ya Nyeri.

Mwingine aliyemchochea sana kwa imani kwamba Kiswahili ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bw Waititu wa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret.

Anakiri kwamba ilhamu ya kuzamia utetezi wa Kiswahili ni zao la kutangamana kwa karibu sana na wahadhiri wake, hasa Bi Rosemary Achilla ambaye alimnoa vilivyo wakati akisomea shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kati ya 2011 na 2013.

Ualimu

Mnamo 1983, Nderitu alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kagumo kusomea Kiswahili, Jiografia na Elimu ya Viungo vya Mwili (P.E). Alifuzu 1985 na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Nyeri Technical. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili mwaka mmoja baadaye na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo ya lugha miongoni mwa wanafunzi na hata walimu wenzake.

Alihamia katika Shule ya Upili ya Moi Nyeri Complex (kwa sasa inaitwa Shule ya Upili ya Rware) mnamo Septemba 1992 na akahudumu huko kwa miaka tisa. Mnamo 2000, alipandishwa cheo na kufanywa Naibu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Ihwa, Nyeri.

Mbali na kumakinikia majukumu ya uongozi na kuwa mstari wa mbele kudumisha viwango vya juu vya nidhamu miongoni mwa wanafunzi, Nderitu alikuwa pia na wajibu wa kuiendesha Idara ya Lugha.

Hamasa ya kutaka kutangamana na wanafunzi kwa karibu mno na katika mazingira ya kiakademia zaidi, ilimchochea kuacha wadhifa wa Naibu Mwalimu Mkuu mnamo Oktoba 2012 na kuwa mwalimu wa darasani tu katika Shule ya Upili ya Riamukurwe, Nyeri. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka sita hadi alipostaafu rasmi mnamo 2018 akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Nderitu aliwahi kuwa mtahini wa Baraza la Mitihani ya Kenya (KNEC) kati ya 1987 na 1991. Tajriba pevu na uzoefu aliojivunia kutokana na utahini wa Karatasi ya Kwanza ya Kiswahili (Insha) ulimwezesha kuzuru shule mbalimbali katika takriban kaunti zote za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCSE.

Aidha, amewahi kuwa mwamuzi na mwendeshaji wa kipindi ‘Sanaa ya Lugha’ kilichokuwa kikitayarishwa na Bw James Kanuri katika runinga ya KBC. Kati ya 2007 na 2017, Nderitu alihudumu katika Jopo la Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala ya Kenya (KICD) lililokuwa na jukumu la kusoma, kutathmini, kuteua na kuidhinisha vitabu vya fasihi vya kutahiniwa katika KCSE Kiswahili.

Uandishi

Nderitu anaamini kwamba uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Mbali na kumpandisha katika majukwaa ya kila sampuli ya makuzi ya Kiswahili, nyingi za insha alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Baada ya kushirikiana na Mwalimu Andrew Watuha kuandika ‘Mwongozo wa Masaibu ya Ndugu Jero’ mnamo 1995, Nderitu alifyatua ‘Mwongozo wa Visiki’ mwaka uo huo. Vitabu hivyo vilichapishwa na kampuni ya Jemisk Cultural Books iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu Wahome Kaimenyi. Kwa sasa anaandaa riwaya kwa matarajio ya kuchapishwa hivi karibuni.

Jivunio

Katika kipindi cha takriban miongo minne ya ualimu, Nderitu amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Yeye kwa sasa ni mshirikishi wa mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) kwa nia ya kuhamasisha umuhimu wa usomaji wa magazeti katika shule za msingi na upili za humu nchini.

Mbali na kuwa Mkuu wa Michezo katika Kaunti ya Nyeri (1988-1993) na Mwenyekiti wa Shirikisho la Uogeleaji la Kenya (KSF) katika Mkoa wa Kati (2011-2013), Nderitu anajivunia taathira kubwa katika makuzi ya sera za lugha na maendeleo ya jamii.

Amewahi kutafsiri Mikataba ya Huduma (Service Charters) ya Kampuni ya Maji ya Usafi wa Mazingira ya Nyeri (NYEWASCO), Bodi ya Huduma za Maji ya Tana na Hospitali ya Outspan katika Kaunti ya Nyeri. Kwa sasa anahudumu katika Baraza la Wazee la kijiji cha Ihururu na ushauri wake umechangia pakubwa maendeleo ya wanajamii kiuchumi, kitamaduni na kisiasa.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Nderitu hujishughulisha na ufugaji wa nguruwe na ng’ombe wa maziwa nyumbani kwake. Isitoshe, anamiliki vyombo vya kisasa vya mawasiliano kwa umma ambavyo hukodishwa kwa ada ndogo. Ana duka ambalo zaidi ya kuuza vyakula vya mifugo, pia hutoa huduma za M-PESA na za Benki ya KCB mjini Nyeri.

Kwa pamoja na mkewe Bi Miriam Wanjiru, wamejaliwa watoto watatu: Salome Wambui, Charles Wanjohi na Carol Muthoni. Wao pia ni walezi wa watoto wawili: Salome na Charles.