Uharibifu wa nzige sasa washuhudiwa katika kaunti 23
VALENTINE OBARA, GEOFFREY ONDIEKI na JOSEPH KANYI
IDADI ya kaunti zilizovamiwa na nzige imefika 23 huku mashirika ya kimataifa yakionya kuhusu uwezekano wa wadudu hao kuongezeka kuanzia mwezi ujao msimu wa mvua utakapoanza.
Ijapokuwa serikali imeonyesha jitihada za kuangamiza nzige, bado kuna wasiwasi kwani wangali wanaendelea kusambaa na pia walitaga mayai mengi katika maeneo waliyoshambulia awali.
Mnamo Jumatatu, Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya alisema unyunyizaji dawa umeanza kufanywa ardhini ili kuharibu mayai na viwiliwili vya nzige kabla wakomae.
Alizidi kusema hakuna nzige wengine walioingia kupitia mipaka ya Somalia, ingawa wataalamu wameonya kuwa nzige huenda wakaja tena nchini kuanzia mwezi ujao kwani kwa sasa wangali wanakomaa Somalia ambako hakuna juhudi zinafanywa kukabiliana nao.
Jumanne, wakazi wa eneo la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu walisema nzige walianza kuingia eneo hilo wiki mbili zilizopita na kufikia jana ndipo wakaingiwa na wasiwasi kwani idadi iliongezeka sana.
Leo nzige walionekana katika Kaunti ya Nyeri ambapo wamezua hofu ya kuharibu mashamba ya kahawa. Wakazi waliona wadudu hao katika kijiji cha Kangurwe.
Idadi kubwa ya nzige waliovamia miti ya kahawa ilifanya hata baadhi ya mimea hiyo kuanguka kwa sababu ya uzani wao.
Kando na kahawa, walivamia pia mimea ya mihogo miongoni mwa mengine mashambani.
Hii imefanya kaunti zilizoshambuliwa kufika 23, ambayo ni sawa na asilimia 49 ya kaunti zote nchini.
Wataalamu kutoka kwa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP), Shirika la kutoa Ilani za Njaa (FEWS NET) na Mamlaka ya Ushirikiano wa Maendeleo Kiserikali (IGAD) zilisema kuna uwezekano mkubwa msimu wa mvua utakapoanza, nzige watataga mayai zaidi na kuendelea kuenea.
“Gharama ya kutoa misaada ya chakula itakuwa kubwa zaidi kuliko ile inahitajika kuangamiza wadudu hao. Kwa hivyo ni muhimu mataifa yajizatiti,” mashirika hayo yakasema katika taarifa ya pamoja.
FAO imeorodhesha Kenya, Ethiopia na Somalia kama mataifa ambayo yamo hatarini zaidi Afrika Mashariki kukumbwa na njaa miezi ijayo kwa sababu ya nzige.
Mbali na Kisumu, wakazi wa Kaunti ya Kirinyaga waliingiwa hofu Jumatatu wakati nzige walipovamia mashamba yao.
Ripoti ya FAO inaonyesha kaunti nyingine iliyoathirika majuzi zaidi ni Kericho ambapo wadudu hao walionekana Jumanne iliyopita.
Katika Kaunti ya Samburu, wadudu hao walivamia upya Kaunti Ndogo ya Samburu Mashariki wakitoka Isiolo.
Takwimu za Serikali ya Kaunti zilisema ekari zaidi ya 70,000 ya mimea na lishe ya mifugo zimeharibiwa kufikia sasa katika kaunti hiyo.
Imefichuka kwamba baadhi ya wafugaji wameanza kuzozania lishe ya mifugo iliyobaki, na kusababisha hofu ya ghasia.
“Jamii kutoka Samburu Mashariki tayari zimeanza kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta lishe na tunahofia hali hii inaweza kusababisha mapigani,” akasema Afisa Mkuu wa Mipango Maalumu katika kaunti hiyo, Bw Daniel Lesaigor.
Kaunti nyingine zilizoathirika ni Kajiado, Makueni, Machakos, Embu, Kitui, Muranga, Garissa, Meru, Isiolo, Mandera, Wajir, Turkana, Pokot Magharibi, Tharaka Nithi, Laikipia, Marsabit, Baringo na Tana River.