• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Safaricom yazindua nambari zinazoanza na 01, Wakenya kuchagua wanazopenda

Safaricom yazindua nambari zinazoanza na 01, Wakenya kuchagua wanazopenda

Na VALENTINE OBARA

KAMPUNI ya Safaricom imezindua mpango mpya ambao utawezesha wateja wapya kujichagulia nambari wanazotaka za simu.

Afisa Mkuu wa maslahi ya wateja, Bi Sylvia Mulinge Jumanne alitangaza mpango huo wakati Safaricom ilipozindua utumizi wa nambari mpya zinazoanza na 01 badala ya 07.

Mwaka uliopita, Mamlaka ya Mawasiliano nchini ilisema ongezeko la wateja wanaotumia simu za mkononi ilisababisha nambari zinazoanza na 07 kuisha.

Nambari mpya za Safaricom sasa zitakuwa zikianza na 0110 au 0111.

“Tunazidi kuwekeza katika kuimarisha huduma ili kutimiza mahitaji ya wateja wetu kwa njia bora zaidi ili kuwaongezea uhuru na uwezo wa mabadiliko,” akasema Bi Mulinge.

Kampuni ya Airtel ilikuwa ya kwanza kutekeleza utumizi wa nambari mpya mnamo Agosti mwaka uliopita, ilipotangaza nambari zake mpya zitaanza na 0100,0101 na 0102.

Safaricom inayoongoza kwa idadi ya wateja nchini imesema sasa ina uwezo wa kuongeza wateja milioni mbili. Takwimu zake zinaonyesha idadi ya wateja wake imefika milioni 34.5.

Kadi mpya zitatolewa kwa wateja bila malipo lakini watahitajika kujaza muda wa mawasiliano ya Sh50 ili kuanza kutumia kadi.

You can share this post!

Mradi wa Ushanga Initiative wawawezesha wanawake...

Wanafunzi wa Kenya walio China wataka usaidizi wa serikali

adminleo