• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wanafunzi wa Kenya walio China wataka usaidizi wa serikali

Wanafunzi wa Kenya walio China wataka usaidizi wa serikali

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wa Kenya walio nchini China wanaendelea kuisihi serikali ifanye juhudi ya kuwarejesha nyumbani.

Bw Jeffery Okundi ambaye ni mwanafunzi katika chuo kimoja Wuhan nchini China anasema kwa muda wa mwezi mmoja sasa wanafunzi kutoka Kenya hawaruhusiwi kutoka nje na kwa hivyo wanashinda ndani ya vyumba vyao mchana kutwa.

“Sisi hapa China tuko katika hali ngumu ya maisha na itakuwa jambo zuri serikali ichukue hatua kabambe kuona ya kwamba masilahi yetu yanapewa kipaumbele,” alisema Bw Okundi.

Katika mahojiano ya moja kwa moja na runinga ya Citizen mnamo Jumanne, Bw Okundi alisema ya kwamba nchi kama Misri na Morocco tayari zimewahamisha raia wao kwa kuwaondosha China.

Alisema tayari masomo yao yamekatiza kwa muda huku wakati mwingi wakiwa wamejifungia ndani ya vyumba.

“Wengi wetu jamaa zetu wamebaki wakiwa na wasiwasi huku wakiwasiliana nasi kila mara wakitaka kujua hali yetu ya kiafya. Nasi tumebaki na hofu kwani hatujui hali hii tutaivumilia hadi lini,” alisema Bw Okundi.

Alisema kwa wakati huu maisha yamekuwa magumu ajabu ambapo hata mtindo wa kula chakula umebadilika.

“Hii ni kwa sababu tunapewa chakula na serikali lakini ni sharti tujipange kwa kula mara moja kwa siku ili tusije tukakimaliza kabla ya kupata kingine,” alisema Bw Okundi.

Alisema vifaa muhimu wanavyopewa ni kama sabuni ya kuoga, dawa ya meno, na chakula cha kujisitiri kwa muda.

Dkt Philip Muthike wa hospitali kuu ya Kenyatta na mwenzake wa kufanya utafiti Dkt Loice Obanjo walisema wageni wengi wanaosafiri kutoka nchi za nje wanafanyiwa vipimo muhimu ili kuthibitisha kama kweli mtu ameambukizwa virusi vya Corona.

“Hata hivyo, ni sharti mgeni yeyote anayeshukiwa kuwa na virusi atengwe kwa muda wa siku 14 kabla ya kubaini kama kweli ameambukizwa,” alisema Dkt Muthike.

Dkt Obanjo alisema kwa sasa ni vyema kujikinga na virusi hivyo kwa kufuata masharti ya kawaida ya kuosha mikono wakati wowote, na kujiepusha na mtu anayepiga chafya ovyo, na ukihisi dalili za joto, na homa isiyo ya kawaida ni sharti kufika hospitali kwa ukaguzi zaidi.

Alisema katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ukaguzi wa kutosha kwa wasafiri wote wanaoingia nchini kutoka nchi za nje hasa China, unafanywa.

Serikali pia imesema mara kwa mara kuwa iko imara kukabiliana na maradhi hayo ambayo kufikia sasa hayana tiba maalumu.

You can share this post!

Safaricom yazindua nambari zinazoanza na 01, Wakenya...

‘Wadau wote sekta ya bodaboda watoe mafunzo kwa...

adminleo