• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Kalonzo sasa ataka Mombasa iwe bandari huru

Kalonzo sasa ataka Mombasa iwe bandari huru

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka, amependekeza jiji la Mombasa ligeuzwe kuwa bandari huru, ili kuondoa mvutano ambao umekuwepo kati ya Serikali ya Kitaifa na wasafirishaji mizigo.

Bw Musyoka alisema kuwa hatua hiyo itamfanya kila mmoja kuwa huru kuendesha shughuli za usafirishaji mizigo, kinyume na sasa ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya pande hizo mbili kuhusu utaratibu wa usafirishaji.

Akitoa mapendekezo yake kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi jana, Bw Musyoka alisema kuwa hatua hiyo ndiyo itahakikisha ukuaji wa uchumi wa eneo la Pwani na nchi nzima kwa jumla.

Kumekuwepo na mvutano mkali kati ya Serikali Kuu na wasafirishaji mizigo, wakiilaumu serikali kwa kuwanyanyasa, kwa kusisitiza kuwa lazima mizigo inayosafirishwa kutoka Mombasa hadi Nairobi isafirishwe kwa reli ya kisasa (SGR).

Mnamo Oktoba mwaka uliopita, wasafirishaji walifanya maandamano jijini humo kulalamikia hatua hiyo, hali iliyofanya wasafirishaji 13 kukamatwa na polisi.

Na ijapokuwa kumekuwepo na juhudi za kusuluhisha mzozo huo kati ya wasafirishaji hao, Serikali ya Kitaifa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, kungali kuna malalamishi ya ubaguzi miongoni mwa wasafirishaji.

“Tunapaswa kubuni jopokazi ambalo litaweka taratibu zitakazohakikisha kuwa Mombasa imegeuzwa kuwa bandari huru. Ni vizuri kwa miundomsingi muhimu kama SGR kuwepo, ijapokuwa pana haja kubuni mazingira ambamo kila mmoja atafaidika kiuchumi,” akasema Bw Musyoka.

You can share this post!

Barclays sasa yaitwa Absa

Vilio katika kaunti baada ya mishahara kucheleweshwa

adminleo