Habari

Utaratibu wa kuajiri walimu Kaskazini Mashariki ugatuliwe, ashauri gavana Roba

February 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na DIANA MUTHEU

GAVANA wa Mandera sasa anashauri utaratibu wa kuajiri walimu ugatuliwe ili kusaidia kumaliza tatizo la uhaba wa walimu katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Akihutubia wanahabari Alhamisi baada ya mkutano na wadau katika sekta ya elimu uliofanyika Mandera, Gavana Ali Roba amesema hatua ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kuwahamisha walimu kutoka eneo hilo iliashiria kuwa serikali imetelekeza sekta ya elimu.

“Tukipewa ruhusa tutafadhili vijana kusoma katika vyuo vya ualimu. Shida si sekta ya elimu bali ni ukosefu wa usalama. Kuna zaidi ya watu 7,000 kutoka sehemu zingine na wanafanya biashara zao bila kutatizwa,” amesema Gavana Roba.

Serikali nayo imesema kuwa itaanzisha mchakato wa kutoa mafunzo kwa vijana waliohitimu katika eneo la Kaskazini Mashariki ili kukabili changamoto zinazokumba sekta ya elimu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika majengo ya GPO Posta, Nairobi, Msemaji wa serikali, Kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema serikali itaweka mfumo wa kuajiri vijana waliohitimu kutoka maeneo hayo.

Msemaji wa serikali Kanali Mstaafu, Cyrus Oguna azungumza na waandishi katika majengo ya GPO Posta, Nairobi. Amesema serikali itatoa mafunzo kwa vijana waliohitimu katika eneo la Kaskazini Mashariki ili kumaliza changamoto ya ukosefu wa walimu. Picha/ Diana Mutheu

Bw Oguna amesema serikali inalenga pia kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Hii ni baada ya TSC kuhamisha zaidi ya walimu 800 kutoka sehemu hiyo wenzao watatu walipouawa kutokana na shambulio linaloshukiwa lilitekelezwa na wapiganaji wa al-Shabaab.

Pia Oguna amesema wataendelea kufanya mikutano na wadau kama vile maafisa kutoka serikali ya kaunti katika eneo hilo, wengine kutoka serikali kuu, viongozi na wenyeji ili watafute suluhu kwa swala nyeti la ukosefu wa usalama.

“Walimu hao hawakutoroka lakini walipelekwa katika maeneo salama. Serikali itapeleka wadumisha usalama wa kutosha katika eneo hilo, ili kuhakikisha usalama wa wenyeji na wageni katika eneo hilo,” amesema Oguna.