Polisi anayelinda ofisi ya Ruto apatikana amefariki
Na MWANDISHI WETU
AFISA wa polisi anayelinda afisi ya Naibu Rais William Ruto ya Harambee Annex jijini Nairobi, Alhamisi alipatikana amefariki nyumbani kwake mtaa wa Imara Daima.
Kulingana na walioshuhudia mwili wa Sajini Kipyegon Kenei ukiondolewa, walisema ulikuwa na majeraha mawili ya risasi kichwani na tumboni.
“Risasi iliyopigwa kichwani ilibomoa ubongo na kuacha alama kwenye paa la chumba. Ile nyingine iliacha jeraha tumboni,” akasema shahidi.
Ripoti zilisema maafisa waliofika wakiwa kwenye gari aina ya Land Cruiser kuchukua mwili kwanza walizuiwa na afisa mwingine anayeishi karibu na nyumba ya marehemu.
Afisa huyo aliwataka wajitambulishe kwa sababu hawakuwa na sare rasmi za polisi na wakamweleza hufanya kazi afisini kwa Naibu Rais na wakathibitisha kwa vitambulisho.
“Maafisa hao walimtaka mwenye nyumba aandikishe taarifa kuhusu kisa hicho,” akasema mdokezi.
Mdokezi mwingine aliambia Taifa Leo kuwa mara ya mwisho afisa huyo kuonekana kazini ilikuwa Alhamisi saa tatu asubuhi.
Majirani waliomfahamu marehemu walikataa kutoa maelezo zaidi kwa kuhofia maisha yao.
Uchunguzi wa polisi na daktari wa kukagua maiti huenda ukatoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo.
Mnamo Jumatano, Dkt Ruto aliagiza maafisa wa usalama katika ofisi yake wabadilishwe.
Pia, alimwandikia Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai barua kuhusu tukio ambapo aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa wiki jana alienda ofisini mwake Harambee Annex wiki iliyopita, kwenye kile kimeibuka kuwa njama ya kutapeli wageni akidai angewasaidia kupata kandarasi ya kuuza vifaa vya kijeshi.
Katika moja ya barua mbili alizoandika, Dkt Ruto alisema wawekezaji wanaohusishwa na kashfa hiyo hawafai kuondoka nchini kabla ya uchunguzi kuhusu vitendo vyao nchini kukamilika.
Maafisa wanne waliokuwa wakilinda ofisi hizo walihojiwa na wapelelezi wanaochunguza tukio hilo.
Alituma nakala za barua hiyo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Ujasusi (NIS) Phillip Kameru na mwenzake wa upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.
Bw Kinoti alisisitiza kuwa washukiwa zaidi watakamatwa kuhusiana na sakata hiyo.