Michezo

HAPO SASA! Arsenal guu moja mbele raundi ya 32-bora Uropa

February 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

STRAIKA Alexandre Lacazette alipachika bao lililowezesha Arsenal kuzamisha Olympiacos 1-0, kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya 32-bora Ligi ya Uropa, Alhamisi.

Lacazette alijaza kimiani krosi safi kutoka kwa beki wa kushoto wa kushuka na kupanda, Bukayo Saka.

Robin van Persie alimmiminia sifa tele chipukizi Saka, 18, ambaye amechangia pasi nane zilizozalisha mabao msimu huu.

Van Persie sasa amemlinganisha na vigogo Ryan Giggs, Dennis Bergkamp na Paul Scholes. “Ryan Giggs alikuwa akichota pasi za uhakika kama hizo. Pia Dennis Bergkamp, Paul Scholes,” Van Persie alieleza runinga ya BT Sport baada ya mchuano huo.

“Ni krosi za kiwango cha juu kabisa. Ni tamu sana. Anafanya kazi ionekane kuwa rahisi, lakini pasi kama hii, nilivyosema, inaweza tu kuchanjwa na wachezaji stadi.”

Aliendelea: “Kwa kweli anatumia nafasi yake vyema. Inafurahisha kuona kazi hiyo inafanywa na kinda ambaye amevalia njuga fursa aliyopewa. Anafanya kazi nzuri sana. Inafurahisha sana kuona kazi yake.”

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta pia ametambua kazi nzuri ya Saka. Amesifu beki huyo Mwingereza akisema baada ya mechi kuwa, ana talanta inayozidi ya beki.

“Tunajaribu kumchezesha katika nafasi ambayo anaweza kuzingirwa na wachezaji wanaofaa katika maeneo yanayofaa,” alisema Arteta.

“Yeye si beki kamili. Ana ujasiri mwingi wa kufanya maamuzi karibu na kisanduku. Nimeridhishwa sana na mchezo wake.”

Bao hilo la ugenini linaweka Arsenal katika nafasi nzuri ya kuingia raundi ya 16-bora.

Katika mechi nyingine ya Uropa usiku huyo, Manchester United ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Club Brugge. Emmanuel Dennis alipatia wenyeji Club Brugge bao katika dakika ya dakika ya 15 kabla ya Anthony Martial kusawazisha dakika ya 36 uwanjani Jan Breydel.

Baada ya mchuano kocha Ole Gunnar Solskjaer alisema: “Ilikuwa mechi ngumu iliyochezewa katika hali mbaya ya anga. Tulipoteza umakinifu mara kadha, lakini hali ya uwanja na mpira zilifanya mambo kuwa magumu.”

Man-United itarudiana na Club Brugge uwanjani Old Trafford mnamo Februari 27.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amelaumu mipira inayotumika kwenye Ligi ya Uropa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Club Brugge.

Kabla ya mechi za marudiano, Arsenal itapepetana na Everton nayo United ilimane na Watford kwenye Ligi Kuu uwanjani Emirates na Old Trafford hapo Jumapili, mtawalia.