• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
DAU LA MAISHA: Vita vyake dhidi ya dhuluma za kijinsia vyafanya awe msimamizi wa kijiji

DAU LA MAISHA: Vita vyake dhidi ya dhuluma za kijinsia vyafanya awe msimamizi wa kijiji

Na PAULINE ONGAJI

VITA vyake dhidi ya dhuluma za kijinsia vimempa umaarufu katika jamii yake.

Kutana na Christine Namunyak, msimamizi wa kijiji cha Archers Post, Kaunti ya Samburu. Namunyak amekuwa sauti kuu katika vita dhidi ya dhuluma za kijinsia na hasa ukeketaji, na hivyo kujizolea heshima.

Ndiposa haishangazi kwamba amepewa wadhifa wa kusimamia kijiji, wadhifa ambao kwa kawaida huhifadhiwa wanaume katika jamii yake. Yeye ndiye mwanamke wa kipekee anayeshikilia wadhifa wa aina hii katika kaunti yake.

“Mimi ndiye msimamizi wa kijiji wa pekee mwanamke. Pia, kuna msimamizi wa wadi mwanamke, ambapo sisi ndio wanawake wa kipekee tunaohudumu pamoja na wanaume,” asema.

Baadhi ya majukumu yake ni pamoja na kuandaa mikutano ya kuhamasisha jamii ambapo amekuwa mstari wa mbele kupaza sauti katika mikutano ya wazee katika vijiji mbali mbali eneo hilo. Aidha, mara kwa mara amekuwa akikusanya wamorani na kuandaa mikutano nao.

Katika mikutano hii, ujumbe anaopitisha hasa ni madhara yanayotokana na ukeketaji.

Kampeni zake zimekuwa zikihusisha kuelimisha vijana kuhusu madhara yanayotokana na ukeketaji, huku nia yake ikiwa kuwarai kuoa wanawake ambao hawajatahiriwa, kinyume na utamaduni.

“Vita dhidi ya ukeketaji kamwe haviwezi kufaulu pasipo kushirikisha pia wavulana kwani ni wao ndio wanapaswa kuoa hawa wasichana wakishakomaa na kuwa wanawake,” asema.

Mbali na hayo, ujumbe wake umekuwa wa kukomesha dhuluma za kijinsia pia miongoni mwa watoto wa kiume.

“Licha ya kuwa wasichana na wanawake kwa kawaida ndio huwa waathiriwa wa dhuluma za kijinsia, wavulana pia wamekuwa wakikumbana na tatizo hili, masaibu yao hayawezi puuzwa,” asema.

Mbali na hayo, kazi yake imehusisha kuwanasihi vijana huku huduma zake zikimpeleka katika vijiji mbali mbali vya kaunti hiyo, kama vile Lombae, Laresoro na Nakwamir miongoni mwa vingine.

Ari yake ya kujihusisha na vita hivi ilitokana na safari yake ngumu katika harakati za kujitafutia elimu.

“Nikiwa msichana mdogo niliajiriwa kama kijakazi na mara kwa mara ningeazima vitabu vya watoto wa mwajiri wangu ili pia nami nisome,” aeleza.

Mazoea haya yaliendelea hadi wakati mmoja alipoamua kujipeleka shuleni mwenyewe. Licha ya kupata ugumu kutoka kwa mwajiri wake, alijikaza na baadaye alibahatika kupata ufadhili uliomwezesha kukamilisha masomo na hata kujiunga na chuo cha mafunzo ya juu na kusomea huduma ya jamiii.

“Ni baada ya hapa ndipo niliona haja ya kusaidia watu katika jamii kwani hata mimi nilisaidiwa,” asema.

Kwa sasa kazi yake ya kueneza ujumbe dhidi ya ukeketaji imemzolea sifa na kumtambulisha miongoni mwa wakazi wa eneo hili. Lakini haimaanishi kwamba safari hii haijakosa changamoto.

Kulingana na Bi Namunyak mtihani mkuu katika kazi yake umekuwa kuishawishi jamii na hasa wazee kwamba ukeketaji una athari katika afya na maisha ya msichana.

“Kwanza kabisa, katika jami yetu mwanamke hapaswi kuzungumza mbele ya wanaume, na hivyo ilichukua muda kabla nianze kuruhusiwa kuwahutubia wazee. Aidha, kizingiti kingine kilikuwa kuwashawishi kutupilia mbali utamaduni huu ambao wameshikilia kwa muda mrefu,” aeleza huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na subira katika vita hivi.

Kulingana naye, suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana sharti liangaziwe ili vita dhidi ya ukeketaji vifaulu.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Alikuwa sauti kuu dhidi ya kansa na...

Mwili wa msichana wapatikana kwenye shimo la maji-taka Lamu

adminleo