Makala

RIZIKI: Kutoka tarishi wa kutumia pikipiki hadi mmiliki wa tuktuk

February 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MIAKA 12 iliyopita baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, Timothy Makutwa alijisajili katika chuo kimoja cha mafunzo ya udereva jijini Nairobi.

Barabaro huyo alinolewa bongo na kimatendo kuendesha magari mbalimbali, ikiwamo malori makubwa.

Timothy alitamani kuwa dereva wa malori makubwa, lakini kwa sababu alikuwa mdogo kiumri hakuruhusiwa.

“Sheria za uchukuzi hazikuniruhusu kuwa dereva wa lori hadi nihitimu miaka inayotakiwa pamoja na tajiriba ya kutosha,” anaeleza.

Gange aliyopata ilikuwa ya uchukuzi, ambapo alihudumu kama tarishi wa kampuni moja Nairobi, kupitia pikipiki.

Mchagua jembe si mkulima, Timothy anasema alifanya kazi hiyo kwa hali na mali. Kilikuwa kibarua chenye changamoto za hapa na pale, na anasema si mara moja, mbili au tatu, alikesha selini kwa anachotaja kama “kukwaruzana na maafisa wa trafiki”.

“Pikipiki yoyote inapoonekana, maafisa wa trafiki huichukulia kama bodaboda. Kuna wakati nilifikishwa kortini kwa kosa dogo tu nikahukumiwa kifungo cha miezi mitatu gerezani au kutoa faini,” Timothy akumbuka, akifichua alitoa faini ya Sh30,000.

Wakati huo alikuwa amepata mchumba na tayari walikuwa wamejaaliwa watoto wawili, hivyo basi alikuwa na majukumu kukithi familia yake.

Licha ya changamoto kibao alizopitia, Timothy anasema alikuwa mwadilifu katika uwekaji akiba. Miaka kadha baadaye katika huduma hiyo, alikuwa ameweka kibindoni kima cha takriban Sh500,000.

Mwaka 2015 aliwekeza katika sekta ya uchukuzi, ambapo alinunua tuktuk mpya iliyomgharimu Sh415,000. Ni sekta ambayo katika siku za hivi karibuni imeonekana kubuni nafasi tele za kazi kwa vijana.

Anasema aliajiri dereva, na mwaka mmoja baadaye aliacha kazi ya uhudumu kama mjumbe na kuingilia kikamilifu uchukuzi kwa njia ya tuktuk.

Kijigari hicho kidogo kinahudumu eneo la Githurai, ambapo husafirisha abiria kati ya mtaa huo na Progressive, Mumbi na Mwihoko.

Kulingana na Timothy pia hukodishwa kusafirisha bidhaa.

Wakati wa mahojiano eneo la Ruaka, Kiambu, ambapo alikuwa amekodishwa kusafirisha vifaa vya ujenzi, Timothy alisema sekta hiyo ina mapato ya haraka.

“Gharama ya kutunza tuktuk ni ya chini mno,” akasema.

Mjasirimali huyo pia anasema gharama ya usafiri na uchukuzi kwa njia ya tuktuk ni nafuu mno ikilinganishwa na magari mengine.

Kwa mfano nauli kati ya Mwihoko na Githurai ni Sh30 – 50. Kuna masafa mengine ya Sh20.

Eneo la Githurai lina zaidi ya tuktuk 300, ambazo zinasifiwa kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi ikiwa ni pamoja na kubuni nafasi za ajira miongoni mwa vijana.

Timothy anasema anapania kuongeza tuktuk moja zaidi, katika maazimio ya ruwaza yake ya miaka mitano ijayo. Ili kuafikia lengo la aina hiyo, Peninah Sianoi mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi anashauri haja kukumbatia uwekaji akiba.

Peninah anasema njia rahisi kuweka akiba ni kujiunga na chama cha ushirika, ndiyo Sacco.

“Sacco zinafahamika kuzalisha riba ukiweka akiba na pia hutoa mikopo kwa riba ya chini,” aelezea, akisisitiza ni muhimu kujiunga kwa makundi ya watu wanaojuana ili kuwekeana dhamana.

Kiwango cha akiba na dhamana ni baadhi ya mahitaji yanayozingatiwa na mashirika ya kifedha kama vile benki na Sacco, kabla kutoa mikopo.