Makamishna wa IEBC waliosalia wapokonywa walinzi na madereva
CHARLES WASONGA na VALENTINE OBARA
MAKAMISHNA watatu waliosalia kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiwemo Mwenyekiti Wafula Chebukati, Jumanne walipokonywa walinzi na madereva wao.
Hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya viongozi mbalimbali, akiwemo Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Aden Duale kutaka IEBC ifagiliwe ili kuteuliwe makamishna wapya.
Meneja wa mawasiliano katika IEBC, Bw Andrew Limo, alisema watatu hao ambao ni Mwenyekiti Wafula Chebukati, na makamishna Boyu Molu na Prof Ayub Guliye, wana haki kupewa walinzi hadi wakati muda wao wa kuhudumia tume utakamilika.
“Kuondoa walinzi wao kunaweza kuhatarisha usalama wa mwenyekiti na makamishna. Hatua hii inadhuru uwezo wao wa kutekeleza majukumu katika tume,” akasema.
Awali, Bw Chebukati alikuwa amepuuzilia mbali wito wa kumtaka ajiuzulu na badala yake akasema inafaa wabunge waweke mikakati ya kupitisha sheria itakayotoa mwongozo wa jinsi ya kuajiri makamishna watakaojaza nafasi zilizoachwa wazi.
“Bunge halijapitisha sheria ya kusimamia jinsi ya kuajiri makamishna kuchukua mahala pa wale wanaoondoka. Hivyo basi, tunaomba asasi husika za serikali zichukue hatua zinazofaa ili kuhakikisha majukumu ya tume hayakwami,” akasema.
Kulingana naye, makamishna Consolata Nkatha Maina (Naibu Mwenyekiti), Dkt Paul Kibiwott Kurgat na Margaret Wanjala Mwachanya ambao walijiuzulu walionyesha hawana uwezo wa kuongoza tume inapokumbwa na matatizo, na pia si wenye moyo wa kukumbatia maoni yanayotofautiana na misimamo yao.
Lakini viongozi walizidi kusisitiza tume hiyo ivunjwe ili iundwe upya.
Waondoke kwa utaratibu
Bw Duale alitaka Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kusuluhisha mzozo katika IEBC kwa kuandaa utaratibu utakaowezesha Chebukati na wenzake kuondoka afisini. Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, William Cheptumo.
Aliwalaumu viongozi wa kidini kwa masaibu yanayoizonga Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akisema waliwapa Wakenya “bidhaa mbovu”, kupitia kwa jopo la uteuzi wa makamishna wa tume hiyo lililoongozwa na wawakilishi wa makundi ya kidini.
“Chebukati aliletwa na viongozi wa kidini. Yeye na wenzake ni “bidhaa mbovu” kwani wanatumia wakati mwingi kuzozana badala ya kufanya kazi,” akasema huku akiunga mkono shinikizo za kumtaka Bw Chebukati na makamishna Prof Abdi Guliye na Boya Molu wajiuzulu.
Hata hivyo, viongozi hao wa kidini waliwasilisha orodha ya watu kadhaa kwa Rais Uhuru Kenyatta, ndipo uamuzi ukafanywa kuhusu aliyestahili kushikilia wadhifa huo.
Wito wa kutaka shughuli ya kuvunja IEBC ianzishwe ulikuwa pia umetolewa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen, na mwenzake wa wachache, Bw James Orengo.
Wawili hao walisema hali ya tume hiyo ilivyo sasa inaashiria kuna uozo ambao unaweza tu kutatuliwa kwa kuunda tume mpya.