Corona: Wavuvi wa kambakoche Lamu wapata hasara kufungwa soko China
KALUME KAZUNGU na MASHIRIKA
WAVUVI wa kambakoche (lobster), Kaunti ya Lamu sasa wanadai soko lao la China limefungwa tangu kuzuka kwa virusi vya Corona ambavyo vimesababisha vifo vya watu 2,463 kufikia sasa huku idadi ya maambukizi ikikaribia watu 80,000.
Covid-19 kama ambavyo virusi hivi vimetajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) – na ambavyo kisa cha kwanza kilikuwa Wuhan katika jimbo la Hubei, China – vimesababisha hatua za kidharura na tahadhari kuchukuliwa ambapo athari hasi za kiuchumi zimeshuhudiwa.
Hali hiyo imesababisha wavuvi wa Lamu kukadiria hasara ya zaidi ya Sh40 milioni katika kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita.
Lamu ina zaidi ya wavuvi 6,000 ambapo kati yao 1000 ni wale wanaotekeleza uvuvi wa kambakoche.
Tangu jadi, wavuvi wa kambakoche eneo la Lamu wamekuwa wakitegemea madalali wa Kichina kutoka Mombasa, ambao wamekuwa wakinunua pato lao kwa bei nzuri kabla ya kusafirisha pato hilo mjini Mombasa na kisha kuelekeza nchini China.
Kilo moja ya kambakoche hununuliwa na madalali hao kwa kati ya Sh3,000 hadi Sh3,500.
Katika mahojiano na ‘Taifa Leo’ Mwenyekiti wa Muungano wa Wavuvi na Madalali, Kaunti ya Lamu, Abubakar Twalib, amesema Jumapili idadi kubwa ya wavuvi wa kambakoche wamelazimika kuacha biashara hiyo hasa tangu soko la China kusitishwa kwa muda.
Kulingana na Bw Twalib, wavuvi wa kambakoche wamelazimika kuuza pato lao rejareja, hali ambayo haiwapi faida.
Bw Twalib amesema kilo ya kambakoche sasa huuzwa kwa bei duni ya hadi Sh500 pekee, hatua ambayo inawafanya wavuvi husika kukadiria hasara kila siku.
“Tunasikitika kwamba tangu maradhi ya Corona yaanze kutatiza nchini China, uvuvi wa kambakoche hapa Lamu umedidimia ambapo ati ya wavuvi 1000, tumebaki na wavuvi wasiozidi 100 pekee,” amesema Bw Twalib akiitaka serikali iwajali.
Mvuvi mtajika wa kambakoche kisiwani Lamu Bw Said Alwy amesema amelazimika kuacha biashara hiyo baada ya kushindwa kustahimili hasara itokanayo na ukosefu wa soko hasa tangu soko la China kufungwa.
“Nilikuwa nikiuza kambakoche wangu kwa madalali wa China, ambapo kwa mwezi nilikuwa nikiingiza kati ya Sh15,000 hadi Sh30,000 lakini sasa ni vigumu kupata angalau Sh5,000 kwa mwezi. Nimeacha biashara ya kambakoche kwa muda sasa,” amesema Bw Alwy.
Naye Bw Baheri Salim ameelezea haja ya serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana na kuwajengea wavuvi wa Lamu kiwanda cha samaki na wanyama wengine wa baharini eneo lao.
Bw Salim pia amesema ni vyema ikiwa serikali itasaidia wavuvi wa Lamu kutafuta soko kwenye mataifa mengine ya ng’ambo mbali na China.
“Ikiwa tutaanzishiwa kiwanda cha samaki na bidhaa za baharini hapa kwetu sidhani haya mateso yanayotukumba kwa sasa yatashuhudiwa. Pia watutafutie soko kwenye mataifa mengine ya nje ili tuendelee kuuza samaki wetu, ikiwemo kambakoche mbali na China,” akasema Bw Salim.
Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa shughuli muhimu Kaunti ya Lamu.