• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
Biashara ya mizinga ilivyomwinua kiuchumi

Biashara ya mizinga ilivyomwinua kiuchumi

NA RICHARD MAOSI

Mchango wa kufuga nyuki ni mkubwa katika azma ya wakulima wadogo kujiongezea kipato, ikiaminika kuwa hakuna kiumbe duniani ambacho kinaweza kufanya kazi kwa bidii kama nyuki.

Katika maswala ya kiuchumi nyuki wana manufaa mengi kwa sababu wanaweza kutoa bidhaa muhimu kama vile asali, nta na masega ambavyo ni vyanzo vya kipato kizuri hususan vijijini.

Licha ya hali hii, maeneo mengi yenye uwezo wa kukuza nyuki hayajastawishwa vyema, jambo linalowaachia watafiti katika jukumu kubwa la kuchunguza, na kuelimisha jamii namna ya kujianzishia miradi midogo ya nyuki.

Ezekiel Mumo Mwanzia kijana mwenye umri wa miaka 27, kutoka eneo la Matuu Kithyoko kaunti ya Machakos kilomita 30 kutoka mjini Machakos ni kielelezo bora kwa vijana wenye ari ya kufanikiwa maishani.

Akiwa msomi wa IT alianzisha mradi kutengeneza mizinga na kufuga nyuki, baina ya 2017-2018 akiwa na lengo la kujiajiri na kuwasaidia vijana wengine wasiokuwa na kazi mtaani.

Jukumu lake kubwa likiwa ni kutengeneza mizinga ya nyuki, kisha akawauzia wakulima wenye nia ya kufuga nyuki, na hatimaye wanapojistawisha akanunua asali kutoka kwao

Mara nyingi Mumo hulazimika kuwatafutia wakulima soko la asali kwa kuwanunulia asali ambayo huuzwa kati ya Sh700 -800 kwa lita moja.

“Katika kipande cha ardhi mita 10 kwa 20 mstatili nimetundika mizinga 14 ambayo inatosha kuzalisha takriban lita 115 ya asali, baada ya kila miezi mitatu,” akasema.

Ambapo kwa mwezi mmoja anaweza kurina lita nane ya asali kutoka kwa mzinga mmoja kila msimu (miezi mitatu).

Akizungumza na Akilimali, alisema lengo lake kuu ni kutengeneza bidhaa zinazoweza kutokana na asali, akisama kuwa bidhaa hii ni yenye manufaa makubwa kwa afya ya binadamu.

Mumo anasema kuwa mara nyingi yeye hutumia maonyesho ya kilimo na makongamano ya wakulima, kuwahamasisha wakulima namna ya kufuga nyuki, ili waweze kupata asali ya kutosha.

Aidha alianzisha mradi wenyewe akiwa na lengo la kuwaleta pamoja wakulima wote wa asali katika soko moja, ili waweze kupata soko la pamoja kwa asali yao ambayo huwaniwa na wateja kutoka Nairobi.

Kwa mwezi mmoja Mumo anaweza kutengeneza mizinga 200 na kuwasambazia wakulima kutoka Ongata Rongai, Makueni, Kitui, Mombasa na Voi.

“Mara nyingi idadi ya watumiaji wa asali ni kubwa kuliko kiwango cha asali inayovunwa kila msimu hivyo basi ni lazima wakulima wa asali waweze kujizatiti ili kufikisha kiwango cha asali kinachohitajika sokoni,” akasema.

Hatua ya kuvuna asali

Mumo anasema asali inaweza kuvunwa kwa kutumia aina ya mtambo unaofahamika kama extractor machine ambapo kila mzinga huwa umewekewa fremu.

Katika hatua ya kwanza anasema tahadhari ya kutosha inastahili kutiliwa maanani wakati wa kuvuna asali ambapo mkulima atahitajika kuvalia glavu na magwanda mazito ya kufunika kila sehemu ya mwili.

Pili aandamane na kibatari kinachofuka moshi ili kuwalewesha nyuki ambao wanaweza kumvamia wakati wa kurina asali kutoka kwenye mzinga kwani kila mzinga hubeba nyuki wengi wanaozaana kila siku.

“Fremu yenye masega inapotolewa huingizwa ndani ya kifaa cha centrifugal na mchanganyiko wa asali na sega unachungwa kwa kutumia kichujio chenye mashimo madogo hadi ndani ya kibuyu,” akasema.

Mumo anasema kuwa hatimaye fremu hurudishwa ndani ya mizinga na asali huweza kupakiwa kwa ajili ya kusafirishwa sokoni kwa ajili ya mauzo.

Mumo anasema kuwa kufikia sasa ametengeneza zaidi ya mizinga 500 kwa wakulima wanaokaa katika kijiji cha Mwatunge eneo la Kithyoko Matuu.

Ambapo wakulima wengi sasa wanaweza kuvuna asali yao na wakajipatia kipato, badala ya kutegemea kilimo cha mahindi ambacho hakijakuwa kikinawiri kutokana na uhaba wa mvua miaka ya hivi karibuni.

Aliongezea kuwa asali kutoka maeneo kame ni bora, kushinda ile inayovunwa kutoka katika mazingira yanayopokea mvua nyingi kila mara.

Hii huenda sambamba na aina ya mimea inayokuwa katika mazingira hayo, kwa mfano miti ya aina ya acacia na maua yenye kutoa nta yenye ladha nzuri yanapatikana kwa wingi katika maeneo kame.

“Miti ya acacia aghalabu inafahamika kwa kutoa asali kwa sababu huwavutia nyuki wengi , asali kutoka hapo ni yenye kiwango cha juu kwa kutoa nta zenye ubora wa aina yake,” akasema.

Mumo anasema baadhi ya faida kutokana na asali ni kama vile kupunguza uzani wa ni wa mwili kwa kuchanganya asali na mdalasini katika viungo vya chakula kama vile chai.

Ugonjwa wa mafua pia unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ulaji wa asali mara kwa mara, mchanganyiko wa asali pia unaweza kusaidia kupunguza uvimbaji wa koo na kukohoa kupita kiasi.

You can share this post!

Walemavu Nakuru wanavyofurahia kucheza voliboli

Jinsi ving’ora vilivyochanganya wakazi

adminleo