• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Wakazi walia nzige wametafuna chakula chote

Wakazi walia nzige wametafuna chakula chote

NA STEVE NJUGUNA

WAKAZI wa Kaunti za Laikipia na Nyandarua wamelalamikia uharibifu mwingi uliotekelezwa na nzige wa jangwani waliovamia mashamba yao na kula chakula chote.

Wadudu hao walitua katika kaunti hizo maarufu kwa shughuli za kilimo cha maua na ufugaji na kuvamia mashamba katika wadi za Igwamiti, Salama, Tigithi, Sipili na Githiga, Kaunti ya Laikipia.

Wadi za Kiandege, Mahianyu na Ndaragwa nazo ziliathirika katika gatuzi la Nyandarua, wadudu hao wakila nyasi, lishe ya mifugo na mimea mingine.

Wakulima kutoka maeneo hayo sasa wametoa wito kwa serikali ya kaunti ishirikiane na serikali ya kitaifa ili kupata suluhu na kuzuia uharibifu zaidi.

Bi Tabitha Wangeci kutoka eneo la Rwathia, Laikipia, ambaye shamba lake lilivamiwa na wadudu hao mnamo Jumapili, alisema walikula mahindi aliyokuwa akiendelea kuyavuna.

“Serikali inafaa kuchukua hatua za haraka na kuwanyuyizia nzige hawa kemikali hatari ili kuzuia uharibifu zaidi,” akasema.

Mkazi mwengine kwa jina Simon Lelendu naye alilalamika kwamba nzige hao walikula lishe yote ya mifugo wake pamoja na nyasi karibu na shamba lake.

“Hawa nzige ni wa ajabu mno. Kando na kula nyasi na lishe, wamewaingiza mifugo wangu hofu kuu. Tunaomba serikali itangaze uvamizi huu wa nzige kama janga la kitaifa,” akaongeza Bw Lelendu.

Wakazi wa Laikipia nao wameingiwa na hofu, wakisema uvamizi wa nzige hao utasababisha ugomvi kati yao na wafugaji ambao maeneo yao pia yamevamiwa.

“Nzige hao wamekula nyasi mno katika eneobunge la Laikipia Kaskazini na tuna hofu kwamba wafugaji kutoka huko watapeleka mifugo yao maeneo mengine ya kaunti. Hii itasababisha uhasama wa kijamii kati ya wakulima na wafugaji,” akasema Bw Alex Gitonga.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo wa kaunti, Bw James Mungere, kundi la nzige hao lilivuka mpaka na kuingia Laikipia kupitia kaunti jirani ya Samburu.

Bw Mungere alisema maafisa wa kaunti wako macho kuhakikisha kemikali inanyunyizwa katika maeneo yaliyovamiwa na wadudu hao.

“Hawa ni nzige wa jangwani na uhai wao hutegemea sana joto jingi. Hawawezi kuishi maisha marefu chini ya hali ya hewa ya kaunti yetu,” akasema Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Nyandarua, Dkt James Karitu.

Wadudu hao wameendelea kuwa kero kubwa nchini huku ikihofiwa kuwa wataangamiza mazao katika maeneo yanayotegemewa kwa ukuzaji chakula nchini.

Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya ameendelea kuahidi kuwa serikali inashughulikia suala hilo kwa kikamilifu, huku wataalam mbalimbali wakijitokeza kuelezea mbinu kadha zinazofaa kutumika ili kuwadhibiti nzige hao.

Wakazi wa Kaskazini mwa Rift Valley pia wameelezea hofu yao baada ya nzige kuvamia mashamba katika kaunti ya Elgeyo-Marakwet. Awali walikuwa wamevamia kaunti jirani ya Pokot Magharibi, lakini idadi hiyo ilionekana kuongezeka kwa kiasi kikubwa

Serikali ilituma ndege kunyunyiza dawa katika maeneo yaliyoathiriwa.

You can share this post!

Hii ‘reggae’ ya BBI nitaizima, aapa Ezekiel...

Dagoretti Mixed na Beijing Raiders mabingwa wa Chapa Dimba...

adminleo