NGILA: Tulinde watoto dhidi ya dhuluma kwenye mitandao
NA FAUSTINE NGILA
MAJUZI nilihudhuria maadhimisho ya Siku ya Usalama kwenye Intaneti yaliyoandaliwa na kampuni ya Facebook ikishirikiana na shirika la Watoto Watch.
Usalama wa watoto mitandaoni ulijadiliwa kwa kina, huku wazazi wakiombwa kufuatilia kwa karibu vifaa watoto wao wanatumia mitandaoni.
Kizazi cha sasa cha watoto kinaishi katika enzi tofauti na vizazi vilivyotangulia na kina fursa nyingi za kupata habari kwenye intaneti huku pia idadi ya simu za kisasa ikiongezeka.
Wanasoma na kutazama matini mitandaoni bila udhibiti wowote, kwani wazazi wao wanaishi katika uchumi unaowalazimu kuwa kazini siku kutwa.
Kuna hatari kuu ya kuwaacha watoto hawa bila yeyote wa kudhibiti wanavyotumia intaneti na ni kweli kuwa watoto wengi wamedhulumiwa mitandaoni bila wazazi wao kujua.
Pia, wamesoma na kutazama video za ngono katika umri huo mdogo, ambazo zimechangia katika kudorora kwa maadili.
Usalama wa simu wanazotumia pia umo hatarini. Kuna uwezekano wa watoto wa umri mkubwa kuchukua simu ya mtoto wako na kuitumia kuchapisha jumbe zisizofaa kwenye akaunti za mitandao ya kijamii za mtoto wako.
Pia video chafu zaweza kupakuliwa kwenye simu hiyo, pamoja na michezo hatari inayoshawishi watoto kujitia kitanzi.
Utovu huu wa usalama huchangia matokeo duni shuleni, ithibati kuwa dhuluma mitandaoni zinaathiri uwezo wao wa kufikiria.
Kuzima maovu haya kwa akili za watoto, Facebook ilielezea kuhusu mbinu kadha ambazo wazazi wanafaa kutumia kuhakikisha watoto wamepata habari zinazowafaa kwenye intaneti.? Kwa kutumia mbinu za kiotomatiki kwenye mitandao, wazazi walitakiwa kuzuia maneno hatari kama ‘ngono’, ‘ghasia’, ‘vita’ na ‘mauaji’, miongoni mwa maneno mengine yanayotishia afya ya akili ya mtoto.
Ingawa Facebook imeweka miaka 13 kama umri wa chini zaidi kwa watoto kumiliki akaunti ya mtandao huo, wafanyakazi wa nyumbani wana muda wa kutosha kumfungulia mwanao wa umri wa miaka mitano akaunti.
Duniani kote, wanaharakati wametilia mkazo haja ya wamiliki wa mitandao ya WhatsApp, Facebook, Twitter, YouTube na Instagram kudhibiti habari zinazochapishwa na watumizi. Bila shaka mitandao hii imebuni njia za kuziba matumizi ovyo ya mitandao.
Hata hivyo, litasalia jukumu la kila mzazi kuhakikisha ameelewa jinsi ya kutumia mbinu hizi ili kulinda wanawe dhidi ya wakora wa mitandaoni wanaovizia akaunti za watoto kwa nia ya kuzidukua.
Pia, wazazi wanafaa kuwafundisha wanao jinsi ya kutumia uso na vidole kama njia ya kuwatambulisha, kwani maneno ya siri yanaweza kudukuliwa kirahisi.
Kwa kuwa shule zimezembea kuwafunza wanafunzi mbinu hizi, na shirika la Watoto Watch likiweza kufikia watoto katika kaunti nne pekee, kila mzazi anafaa kutumia mwongozo wa usalama wa habari mitandaoni kulinda vizazi vijavyo dhidi ya madhara haya.