• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
AFYA: Usikimbilie vidonge madukani, nenda kwa daktari afanye ukaguzi

AFYA: Usikimbilie vidonge madukani, nenda kwa daktari afanye ukaguzi

Na BENSON MATHEKA

Wataalamu wa afya wanaonya watu dhidi ya kutumia vidonge vya kuongeza nguvu za kiume wakisema ni hatari kwa afya na maisha.

Wanasema ni makosa kuuzia mtu dawa hizi madukani bila ushauri wa daktari. ?Wanaozitumia bila ushauri wa daktari wanajiweka katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya na hata kifo.

“Vidonge vya kuongeza nguvu za kiume vina matatizo mengi ya kiafya kwa wanaozitumia bila ushauri wa daktari. Wengi wanaozitumia hawana matatizo yoyote ya kiafya. Wanachotaka ni kuonyesha ubabe wao wa kutekeleza tendo la ndoa. Zinapaswa kutumiwa kwa ushauri wa daktari na watu ambao wamefanyiwa uchunguzi wa kimatibabu,” asema Dkt Philip Mule wa hospital ya Penda, Nairobi.

Kulingana na utafiti uliochapishwa katika jarida la Journal for sexual health baadhi ya vidonge watu wanavyonunua madukani wakinuia kuongeza nguvu za kiume havifanyi kazi wanavyofikiria na ni hatari kwa maisha yao.

Utafiti huo unasema kwamba serikali za mataifa mengi hushindwa kuweka sheria za kudhibiti matumizi ya dawa hizo. Wanaume wengi walioshirikishwa kwenye utafiti huo walikiri kutumia vidonge vya kuongeza nguvu za kiume bila kujua zinavyoathiri afya zao.

“Hii ni kwa sababu kuna sheria dhaifu za kuthibiti matumizi ya dawa hizi,” unasema utafiti huo. ?Dkt Mule anasema wanaouza dawa hizi hudai kuwa hazina madhara kwa mwili kwa sababu lengo lao ni kupata faida.

“Kuna wanaodai kuwa ni virutubishi (supplements) ilhali zimegunduliwa kuwa na chembechembe za Viagra, dawa iliyo na madhara mengi ikitumiwa bila ushauri wa daktari,” asema Dkt Mule.

Wataalamu wanasema hata vidonge vinavyouzwa mitaani vya kusisimua wanaume kimapenzi ni hatari.

“Vidonge vingi havijabainishwa kupitia uchunguzi wa kisayansi kuwa na uwezo wa kuongeza nguvu za kiume,” wasema utafiti uliochapishwa katika jarida la Journal for sexual health.

Wataalamu wanasema wanaotumia vidonge hivi bila ushauri wa daktari hujiweka katika hatari ya kupata maradhi ya moyo, figo na ini. Anasema inasikitisha vijana wa umri wa miaka ishirini wanatumia vidonge vya kuongeza nguvu za kiume.

“Vijana wanaotumia tembe za kuongeza uwezo wao wa kufanya mapenzi wanajiweka katika hatari ya kufupisha maisha yao,” asema Dkt Mule.

Wataalamu wanaonya kuwa vidonge vya kuongeza nguvu za kiume vinaweza kupokonya mtu uwezo wake asilia wa kutekeleza tendo la ndoa.

“Mtu anaweza kugeuka mtumwa wa vidonge hivi. Anashindwa kabisa kutekeleza tendo la ndoa asipovitumia,” asema Dkt Mule.

You can share this post!

AFYA: Hofu ya wanaume ‘mlingoti’ kukosa kusimama wima...

AFYA: Jinsi ya kubaini na kujilinda dhidi ya maradhi ya...

adminleo