• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
GWIJI WA WIKI: Isaac Were

GWIJI WA WIKI: Isaac Were

Na CHRIS ADUNGO

FURAHA au ustawi wa mwanadamu huwa umejengwa katika misingi ya kuhitajiana. Kuwathamini watu wengine ni siri kubwa ya kufanikisha ndoto zako za maisha na za kitaaluma.

Ukamilifu katika maisha hutegemea mchango wa marafiki wanaokuzingira. Wateue wasiri wako kwa makini sana. Pima mizani ya maisha na jaribu kuongeza marafiki pale panapostahili. Jijali kwa kuwa asiyejali hupata ajali! Nidhamu na imani ni kati ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya mtu.

Bila kuvumiliana, wanadamu hatuwezi kupiga hatua yoyote ya kusonga mbele. Jifunze kutokana na yaliyopita ndipo uweze kujenga ya sasa na kuyakabili yajayo. Salia imara katika jitihada za kufikia malengo yako, uwe mkakamavu, mwenye bidii na mwaminifu katika shughuli zako.

Huu ndio ushauri wa Bw Isaac Were Oduori – mwandishi chipukizi wa fasihi, mlezi wa vipaji na mfanyabiashara ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Louis Butula Boys, Busia.

MAISHA YA AWALI

Were alizaliwa mnamo 1967 katika kijiji cha Randago, eneo la Busiada, Kaunti ya Busia akiwa mtoto wa tano katika familia ya marehemu Bi Joyce Khadudu na marehemu Mzee John Were.

Alipata malezi ya awali katika eneo la Tengeru viungani mwa mji wa Arusha, Tanzania. Huko ndiko alikokuwa akiishi baba yake mzazi wakati akiwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Simuli, Busia alikosomea kati ya 1975 na 1981. Alijiunga na Shule ya Upili ya Bukhalarire, Busia mnamo 1982, akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCE) mwishoni mwa 1985 kisha kujisajili kwa masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’.

UALIMU

Were alianza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Bukhalarire baada ya kukamilisha mtihani wa kidato cha sita mnamo Septemba 9, 1986. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka sita kabla ya kujiunga na Chuo cha Walimu cha Shanzu, Mombasa mnamo 1993.

Baada ya kufuzu, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma kufundisha katika Shule ya Msingi ya Bukhakhala, eneo la Bumala, Busia mnamo 1994. Aliteuliwa kuwa Naibu Mwalimu Mkuu shuleni humo mwanzoni mwa 1998.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Historia) mnamo 2000. Alifuzu mwanzoni mwa 2006 na kurejea kufundisha katika Shule ya Msingi ya Bukhakhala.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Busiada Girls, Busia mnamo 2008. Miaka miwili baadaye, alirejea katika Chuo Kikuu cha Maseno kusomea shahada ya uzamili chini ya uelekezi na usimamizi wa Profesa Florence Indede, Profesa Ernest Sangai Mohochi na Dkt Nixon Nabeta Sangili.

Maamuzi yake ya kusomea shahada ya umahiri ni zao la kuchochewa na rafikiye mkubwa, Bw Felix Mawasi.

Mnamo 2012, Were alijiunga na Shule ya Upili ya Sigalame, Busia alikoshirikiana na mwalimu Balala Luvaga na Bw Osinya Okumu kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Butula Boys mnamo Januari 2017 na kupokezwa jukumu la kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Aliushikilia wadhifa huo hadi mwishoni mwa 2018.

Were anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Butula Boys ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotolewa

Baadhi ya walimu hao ni Makarios Makwata, Caren Achieng, Celestine Obam, Derrick Efumbi, Chadwick Obwini na Edwin Omoding ambaye ni Mkuu wa Idara.

KICHOCHEO

Were anatambua upekee wa mchango wa wazazi na walimu wake katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo na kumhangaikia kwa hali na mali.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa pakubwa na Bw Aggrey Musoga na Bi Sylvia Wewa waliomfundisha katika shule ya sekondari. Hawa walitangamana naye kwa karibu sana na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha ilhamu na kariha ya kukichapukia Kiswahili.

“Nilivutiwa mno na umahiri wa walimu hawa, nikatamani sana ije siku ambapo nami ningekuwa na umilisi mkubwa wa lugha, nikisarifu Kiswahili kama wao.”

Akiamini kwamba kinolewacho hupata na ukiona vyaelea vimeundwa, Were alijitolea kwa udi kujifunza Kiswahili na kukitetea vilivyo. Utashi wake katika Kiswahili ulichangiwa na washairi Abdallah Baruwa, Hassan Mwalimu Mbega na Abdallah Mwasimba.

Hamasa zaidi ilitokana na mchango wa wasomi waliokuwa wakiendesha kipindi ‘Lugha Yetu’ katika KBC Redio. Hawa ni pamoja na marehemu Profesa Jay Kitsao, Dkt Ayub Mukhwana, Profesa John Habwe na Profesa Ireri Mbaabu.

UANDISHI

Were anaamini kwamba uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili.

Mbali na kumpandisha katika majukwaa ya kila sampuli ya makuzi ya Kiswahili, nyingi za insha, mashairi na hadithi alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Kwa sasa anaandaa mikusanyiko ya hadithi za watoto na miswada ya ushairi kwa matarajio kwamba kazi hizo zitachapishwa hivi karibuni.

JIVUNIO

Tajriba pevu na uzoefu mpana unaojivuniwa na Were katika taaluma ya ualimu umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Were amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake, anapania pia kuweka hai ndoto za kuwa mmiliki wa vituo na taasisi mbalimbali za elimu ya chekechea zitakazowapa watoto malezi bora zaidi ya kimsingi katika ulingo wa kiakademia.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Were hujishughulisha pia na biashara ya kutoa huduma za usafiri wa teksi.

Kwa pamoja na mkewe Bi Safina Ramadhan ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Bukhalarire, wamejaliwa watoto watatu: Clifford Barrack Oliech, Neema Khadudu na Sanford Wamukoya Alvin.

You can share this post!

AFYA: Kucheza na sabuni kwaweza kumletea mtoto asthma

MOKUA: Haja ya kuteua kozi kwa kuzingatia vigezo...

adminleo