Habari

Coronavirus inavyohangaisha Wakenya

February 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

UGONJWA wa Coronavirus uliochipuka nchini China mnamo Desemba mwaka uliopita, sasa unatishia kuathiri maisha ya Wakenya wanaotegemea taifa hilo kibiashara.

Wafanyabiashara waliozungumza na Taifa Leo walifichua kwamba biashara zao zimo katika hatari ya kufungwa, huku wafanyakazi wa viwanda mbalimbali vinavyotegemea nchi hiyo pia wakihofia kusimamishwa kazi kama hali haitabadilika hivi karibuni.

Kutokana na vikwazo vya usafiri pamoja na hofu kubwa kuhusu ugonjwa huo, imekuwa changamoto kwa wafanyabiashara kuagiza bidhaa wanazohitaji kutoka China.

Kenya imekuwa ikiagiza bidhaa nyingi kutoka China kwa miaka kadhaa sasa.

Idara ya Takwimu za Kitaifa nchini (KNBS) inasema katika miezi sita ya kwanza mwaka wa 2019, Kenya iliagiza bidhaa zinazogharimu Sh169.6 bilioni kutoka nchi hiyo ya Asia.

Bi Varinia Luvega ambaye hufanya biashara ya kuagizia wateja wake bidhaa kutoka China, amekuwa akihangaika tangu Januari.

Alianza biashara hiyo mwaka uliopita alipofutwa kazi na hali ilivyo sasa inamkosesha matumaini ya kuistawisha alivyokuwa amepanga.

“Biashara yangu imeanguka. Nimeshindwa kuagiza chochote. Tunasubiri tu tuone vile kutakavyoenda,” akasema, akieleza kuwa mpango wake wa kuaongeza wateja na kuagiza bidhaa kila mwezi sasa umekwama.

Kulingana naye, huwa rahisi kuagiza bidhaa kutoka China kwani si lazima mfanyabiashara aagize furushi zima, kwa mfano la nguo au viatu, bali wanaweza kuagiza tu idadi ambayo mteja anataka.

Hii ni tofauti na ilivyo katika mataifa mengine ya kigeni.

“Wauzaji wengi China sasa hawafanyi kazi. Wale wachache waliopo wanasema watahitaji angalau siku 15 kabla bidhaa ziondoke China. Tutalazimika kusubiri kwa muda zaidi kabla bidhaa hizo kufika Kenya,” akaeleza.

Alisema kwa kawaida, shughuli nzima ya uagizaji bidhaa hadi zifikie wateja hukamilika kwa muda usiozidi wiki tatu.

Ijapokuwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilifafanua kwamba hakuna hatari ya maambukizi mtu akipokea bidhaa kutoka China, imebainika kuwa madalali wa kusimamia taratibu za kupitisha mizigo ya kibiashara katika viwanja vya ndege pia wanakumbwa na vikwazo kuhusu mizigo inayotoka China.

Kwa msingi huu, biashara yao imeathirika kwani bidhaa nyingi zilikuwa zikitoka katika nchi hiyo.

Bw Dancan Wasilwa, ambaye ni mmiliki wa duka la Trendy Designer Wear jijini Nairobi, ana wasiwasi kwani bidhaa zake zinakaribia kuisha katika stoo.

Yeye ni mmoja wa mamilioni ya vijana Wakenya walioamua kukumbatia ujasiriamali mara walipokamilisha elimu ya Chuo Kikuu kutokana na uhaba wa ajira unaokumba nchi.

Lakini ameipa biashara yake miezi minne kabla aifunge endapo ulimwengu utashindwa kuangamiza coronavirus.

Ijapokuwa anakiri kwamba kuna mataifa mengine ambapo anaweza kuagiza mavazi ya kuuza dukani mwake, alisema itakuwa changamoto kwani wao hupendelea China kwa sababu bidhaa ni za bei ya chini na pia taratibu zao za uagizaji ni rahisi.

Vilevile, nchi nyingine ambazo angetegemea ni za ukanda wa Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali ambapo Coronavirus imeenea katika siku za hivi punde.

“Bidhaa nilizo nazo sasa zinaweza kudumu kwa miezi minne hivi. Tunawazia hatua nyingine lakini zitatugharimu sana. Huwa tunapata wateja wengi wakati bidhaa zinapoweza kuuzwa kwa bei ya chini,” akasema.

Biashara zinazotegemea uagizaji vitambaa kushonea nguo pia zimeathirika. Duru katika kiwanda cha EPZ kilicho Athi River zilisema wafanyakazi wameanza kuhofia kusimamishwa kazi karibuni kama hakutapatikana njia ya kuagiza vitambaa.

Viwanda vya kushona nguo nchini hutegemea sana vitambaa kutoka China, Hong Kong, Sri Lanka na mataifa mengine ya Asia, Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali.

Sekta ya vifaa na mitambo ya kielektroniki pia haijasazwa.

Bi Anne Munderu anayefanya kazi katika kampuni ya Raerex East Africa iliyo Nairobi, alisema wamepata changamoto tangu Januari.

Kampuni hiyo hufanya kazi ya kusambaza na kutengeneza vyombo vya kutia joto au baridi chumbani.

“Hatuna namna. Watu wanajua kile kinachoendelea lakini wateja hawapendi kazi zao zikicheleweshwa. Kuna kazi nyingi ambazo tumelazimika kusitisha na ni vigumu sana kueleza wateja hali inayotukumba,” akasema.

Zaidi ya hayo, alifichua kuwa kampuni hiyo inayoajiri wafanyakazi takriban 100 ilikuwa tayari imelipa wauzaji wa China kwa vifaa walivyohitaji.

“Ukishalipia bidhaa kwa asilimia mia moja, utawezaje kurudi useme urudishiwe pesa zako? Maelewano yetu ni wazi kwamba hakuna kurudishiwa pesa ukishalipia bidhaa,” akasema.

Aliongeza: “Kwa sasa ni vigumu pia kuwasiliana na baadhi ya wauzaji ambao tulikuwa tumewalipa. Hatujui hata kama watawahi kufungua tena biashara zao.”

Wiki iliyopita, ilifichuka kuwa wavuvi wa samaki aina ya kambakoche katika Kaunti ya Lamu wanakadiria hasara kubwa huku baadhi yao wakiamua kuachana na biashara hiyo, kwani soko kubwa walilotegemea lilikuwa China.

Mbali na bidhaa, wataalamu Wakenya wanaotoa huduma kama vile za ushauri wa kibiashara na utafsiri waliambia Taifa Leo malipo yao yamechelewa tangu mkurupuko wa coronavirus ulipozidi.

Takwimu za mwisho kutoka WHO zinaonyesha kulikuwa na maambukizi 79,331 ya coronavirus ulimwenguni kufikia jana. Kati ya idadi hii, maambukizi 77,262 yalikuwa China ambapo vifo 2,595 vimethibitishwa.

Maambukizi 2,069 yalikuwa katika mataifa 29 yaliyo nje ya China ambapo vifo 23 viliripotiwa.