• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Sonko hajaponyoka

Sonko hajaponyoka

VALENTINE OBARA na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko hajaponyoka masaibu tele yanayomwandama licha ya kuikabidhi serikali ya Rais Uhuru Kenyatta sehemu ya uongozi wa kaunti yake.

Kwenye maelewano yaliyofanywa katika Ikulu ya Nairobi, Bw Sonko aliikabidhi Serikali Kuu usimamizi wa idara muhimu zaidi za kaunti ikiwemo ya afya, uchukuzi, ujenzi na mipango ya kaunti.

Jumatano, ilibainika kuwa mpango wa kumng’atua uongozini utaendelea hadi tamati.

Wakati huo huo, alipata pigo kortini wakati Hakimu Mkuu Douglas Ogoti alipokataa kufutilia mbali kesi ya ufisadi wa Sh357 milioni.

Kupitia kwa mawakili wake, Bw Sonko alikuwa amejitetea kwamba Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilichunguza akaunti zake katika benki tano bila idhini yake, na hivyo kukiuka haki zake za usiri.

“Mahakama hii inakubaliana na maagizo ya awali ya Mahakama ya Juu kwamba si lazima mtu kuarifiwa akaunti zake za benki zikichunguzwa,” alisema Bw Ogoti.

Katika Bunge la Kaunti, Kiranja wa Wachache Peter Imwatok, ambaye ndiye mwasisi wa mpango wa kumng’oa Sonko mamlakani alisema gavana huyo alikuwa ashapewa muda wa kutosha kujirekebisha.

Alisema sasa madiwani lazima watekeleze jukumu lao la kikatiba.

“Sisi tunataka uongozi mpya katika kaunti hii. Tulimpa muda mrefu kujirekebisha na tukamwambia hii kaunti si mali yake ya kibinafsi,” akasema.

Kulingana naye, hatua ya gavana huyo kukabidhi serikali kuu baadhi ya majukumu imethibitisha amelemewa na kazi aliyopewa na wapiga kura wa Nairobi.

“Mojawapo ya vigezo vya kutaka kumng’oa mamlakani ilikuwa ni kuhusu kutowajibika katika majukumu yake. Katiba inasema gavana ndiye mkuu wa kaunti. Kazi yake ni kusimamia huduma zilizogatuliwa. Ikiwa sasa hana tena majukumu hayo, mbona aendelee kuwa uongozini?” akauliza diwani huyo wa Wadi ya Makongeni.

Endapo madiwani wanaounga mkono mpango huo watafaulu, Bw Sonko atakuwa gavana wa pili kutimuliwa baada ya Bw Ferdinand Waititu aliyeng’olewa Kiambu.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bi Beatrice Elachi alikuwa amempa gavana huyo hadi Jumatatu ijayo kujitetea dhidi ya madai yaliyotolewa dhidi yake.

Kando na kushindwa kutekeleza majukumu yake, madai mengine yaliyowasilishwa na Bw Imwatok ni kuhusu kukataa kumchagua naibu wake tangu 2018, ubadhirifu wa mali ya umma na kufuta kazi maafisa wa kaunti kiholela kwa hali inayoathiri utendakazi.

Hatua ya Bw Sonko kupeana majukumu yake kwa serikali kuu iliibua hisia mseto miongoni mwa viongozi, mawakili wa masuala ya kikatiba, wadadisi wa kisiasa na wananchi kwa jumla kwani ni mara ya kwanza hali aina hii kuwahi kushuhudiwa tangu ugatuzi ulipoanza kutekelezwa mnamo 2013.

Bi Elachi alisema Bw Sonko amedhihirisha anajali maslahi ya wakazi wa Nairobi kwani shughuli zingekwama endapo atang’olewa mamlakani na hakujapatikana naibu gavana.

Alisema hivi karibuni, mswada wa fedha utapitishwa na kama hakuna gavana kuuidhinisha, ingemaanisha huduma zote muhimu zingekwama.

“Ukitazama jinsi hali ilivyo Nairobi, hatua hii imezuia taabu katika kaunti. Ninamshukuru gavana kwa vile hakuzingatia maslahi yake ya kibinafsi bali pia ya umma,” akaeleza.

Alisema hatua hiyo haimaanishi serikali yote ya kaunti imevunjwa, hivyo basi madiwani wana haki kutekeleza majukumu yao kama kawaida.

Kwa upande mwingine, alisema mawaziri wa kaunti wanaosimamia idara zilizokabidhiwa kwa serikali kuu watatarajiwa kufanya kazi chini ya mawaziri wa serikali kuu.

You can share this post!

SEKTA YA SUKARI: Ripoti ya kufufua sekta ya sukari yatoa...

AKILIMALI: Ng’ombe wa kisasa siri yake ya maziwa tele

adminleo