Kenei alikufa kwa risasi moja shingoni – Daktari
NA CECIL ODONGO
Mwili wa marehemu Sajini Kipyegon Kenei, ambaye kifo chake kimezingirwa na utata, jana ulifanyiwa uchunguzi jana lakini haikubanika iwapo alijitia kitanzi ama aliuawa na mtu mwingine.
Mwanapatholojia Mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alifanya upasuaji huo katika hifadhi ya maiti ya Chiromo, na akathibitisha kwamba marehemu alipigwa risasi moja kwenye shingo na ikapitia kwenye kipaji cha uso.
Marehemu Kenei alikuwa akihudumu katika afisi ya Naibu Rais William Ruto ya Harambee Annex Complex jijini Nairobi, na alipatikana amefariki nyumbani kwake mtaani Imara Daima mnamo Alhamisi wiki jana.
“Tumefanya upasuaji na tunaweza kusema kwamba marehemu Kenei aliaga dunia kutokana na risasi moja iliyopigwa kwa karibu shingoni. Risasi hiyo ilipenya na kutokea kwenye kipaji cha uso. Hatujabainisha iwapo ni kijiua ama aliuawa na mtu mwingine,” akasema Dkt Oduor.
“Kwa kuwa kuna uchunguzi unaoendelea, tumechukua sampuli ambazo zitafanyiwa uchunguzi zaidi na baada ya hapo ndipo tunaweza kufahamu ukweli kuhusu kilichosababisha mauti yake,” akaongeza.
Alisema mwili huo ulikuwa umeanza kuoza, ishara kwamba marehemu aliuawa siku moja au mbili kabla kupatikana kwa mwili wake.
Kwenye upasuaji huo, serikali iliwakilishwa na madaktari wawili huku familia ya Bw Kenei ikiwa na madaktari watatu.
Kabla ya upasuaji kufanyika, familia ya marehemu ikijumuisha babake, mkewe na wanafamilia wengine waliruhusiwa kutazama mwili huo.
Huzuni iliyokuwa nyusoni mwao ilikuwa dhahiri baadhi wakizimia kutokana na uchungu wa kumpoteza mpendwa wao.
Makachero kutoka Idara ya uchunguzi wa makosa ya uhalifu bado wanaendeleza uchunguzi wao kwa lengo la kuhakikisha kwamba iwapo afisa huyo aliuawa basi waliosababisha mauti yake wananyakwa.