• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Dadaye Raila aachiliwa kuhusu kesi ya uchochezi

Dadaye Raila aachiliwa kuhusu kesi ya uchochezi

Na BRENDA AWUOR

MAHAKAMA ya Kisumu jana ilitupilia mbali kesi iliyomhusisha aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisumu Bi Ruth Odinga na Seneta wa Kisumu, Bw Fred Outa, na uchochezi na uharibifu wa vifaa vya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hakimu Mkuu, Bw Peter Gesora, aliamuru kuwa washtakiwa hao wawili pamoja na mwakilishi wa wadi ya Kondele, Bw Joachim Oketch, Bw Francis Odhiambo na Bw Constance Ingutie wako huru.

Kwenye uamuzi wake, alisema kwa muda wa miaka mitatu ambapo kesi hiyo iliendelea, ilikosa mwelekeo.

”Hakuna ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa mambo. Na kwa kuwa hakuna yeyote aliyetoa ushahidi kortini kuhusu kisa hiki, ninaamuru wote kuwa huru,” hakimu akasema.

Walishtakiwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa kuwa ya IEBC pekee na kuzuia afisa mmoja wa IEBC kutimiza wajibu wake.

Kisa hicho cha Oktoba 2017, kilisababisha kuharibika kwa vifaa vya IEBC. Watano hao pia walishtakiwa kwa kosa la wizi wa viti 94 vya plastiki na mahema ya thamani ya Sh92,500.

Seneta Outa pia alishtakiwa kutumia matamshi ya uchochezi katika kituo cha kupiga kura kilichoko katika wadi ya Milimani.

“Bomoa kisha haribu hii mali ya tume ya uchaguzi na mipaka na mahema,” karatasi yenye mashtaka ilinukuu. Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo.

You can share this post!

Mlima Kenya wasilazimishwe kumpigia Ruto kura 2022 –...

Tunahitaji mdahalo kung’amua mimba ya mapema...

adminleo