Tunahitaji mdahalo kung'amua mimba ya mapema ilipoanzia – Ole Kina
Na DIANA MUTHEU
VIONGOZI wameomba vijana wapewe elimu kuhusu maswala ya uzazi ili waweze kujiepusha kupata mimba za mapema.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi, Prof Sam Ongeri, Seneta wa Kisii alisema kuwa elimu itawasaidia vijana kuelewa madhara ya mimba za mapema.
“Elimu itawapa wasichana ujuzi ambao watatumia kujichumia riziki badala ya kujihusisha na ngono za mapema ili kupata bidhaa muhimu kama sodo. Pia, vijana wataweza kujiepusha na ngono za mapema ambazo huwafanya kuwa wazazi kabla hawajajipanga kimaisha,” akasema Prof Ongeri.
Seneta huyo alisema kuwa tatizo hili linafaa kukabiliwa kwa kutumia mbinu mpya. Alisema vijana, wazazi, walimu, viongozi wa kidini, wadau kama vile wizara ya afya na elimu na jamii nzima wanafaa kuhusika katika vita dhidi ya mimba za mapema.
“Siku zimebadilika, teknolojia imekua na hali ya maisha pia imebadilika. Tunafaa kutumia mbinu tofauti kumaliza tatizo hili ambalo linaathiri kaunti zote nchini,” akasema.
Kulingana na ripoti ya 2014 ya Utafiti kuhusu Hali ya Afya katika Maeneo Mbalimbali Nchini (KDHS), Kaunti ya Narok iliongoza kwa idadi ya wasichana waliopata mimba wakiwa wangali wachanga.
Seneta wa Narok, Ledama Ole Kina aliiomba wizara ya afya kujenga vituo zaidi vya afya kusaidia wasichana katika maeneo wanapoishi Wamaasai bila kuzingatia sheria kuwa lazima kuwe na watu 5,000 katika sehemu moja ndipo hospitali ijengwe.
“Inasikitisha Kaunti yetu kutajwa kama inayoongoza kwa visa vya mimba za mapema na mwaka wa 2018 wasichana zaidi ya 15,000 waliathirika. Watoto hawa ndio wanategemewa kuendeleza uchumi wa kaunti. Hivyo, viongozi wote wanafaa kuzungumza na jamii ili wajue shida ilianzia wapi,” akasema Bw Ole Kina.
Seneta Ole Kina aliomba jamii isiwatenge wasichana hawa bali wasaidiwe ili warejee shuleni na pia watoto wao wapewe malezi mema.
Prof Margaret Kamar, Seneta wa Uasin Gishu alisema serikali iwe na mpango wa kutoa sodo kwa wasichana wote hata walio katika mitaa ya mabanda na wale wasiokuwa na makao.
Kulingana na KDHS, sababu kuu za mimba za mapema ni umaskini, ukosefu wa elimu kuhusu uzazi, matumizi ya dawa za kulevya, tamaduni potovu na matumizi mabaya ya teknolojia.
Mimba za mapema hufanya wasichana kupata changamoto wanapojifungua kama vile fistula na hata kuwalazimu wasiendelee na masomo.
KDHS ilipendekeza kuwa serikali iwekeze katika mchakato wa kuhakikisha wasichana wanahudhuria shule ya msingi, upili hadi vyuo vikuu au vile vya anuwai. Pia, elimu kuhusu uzazi ijumuishwe katika silabasi.
Pili, wahudumu katika vituo vya afya waliombwa waunde mazingira yanayowezesha vijana kuongea kuhusu matatizo yao, na tembe za kuzuia mimba zilitolewe bila malipo.
Pia, ilipendekeza kuwa sheria zote za kulinda watoto kutokana na vitendo vya ngono vifuatiliwe na jamii ihamasishwe zaidi kuhusu tamaduni potovu kama vile ukereketaji wa wasichana na madhara yake.