• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
Coronavirus: Saudia yasitisha safari za Mecca

Coronavirus: Saudia yasitisha safari za Mecca

Na AFP

SAUDI Arabia Alhamisi ilisitisha utoaji wa viza kwa mahujaji wanaotaka kuzuru Mecca kutokana na hofu ya virusi vya corona, wizara ya Mashauri ya Kigeni imesema.

Serikali “imesimamisha kwa muda wageni kuja nchini kwa sababu ya Umrah na kuzuru Msikiti wa Nabii, taarifa kutoka wizara hiyo ilisema, ikirejelea safari za hijja ambazo hufanywa wakati wowote.

Umrah huvutia maelfu ya Waislamu kutoka pembe zote za ulimwenguni kila mwezi. Wizara hiyo ilifafanua kuwa imesimamisha utoaji wa viza kwa watalii kutoka mataifa ambayo yanakabiliwa na “hatari” ya kupatikana na virusi vya Corona.

Saudi Arabia, ambayo kufikia sasa haijaripoti kisa chochote cha maambukizi ya virusi hivyo, imeelezea hofu kutokana na kusambaa kwake katika mataifa jirani. Hata hivyo, ilieleza kuwa marufuku hiyo (ya utoaji visa vya usafiri) ni ya muda tu. Lakini haikusema ni lini itaondolewa.

“Serikali imeamua kuchukua hatua hizi za tahadhari; kuzima kuingia kwa wageni kwa ajili ya “umrah” na kutembelewa kwa Msikiti wa Mtume, kwa muda,” taarifa hiyo ilieleza.

Mataifa ya ukanda wa Ghuba tayari yametangaza mikakati kadhaa, ikiwemo kusitisha masomo au kufungwa kwa shule, ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, hasa kutokana na watu waliotoka Iran.

Hata hivyo, Serikali ya Saudi Arabia haikutoa maelezo kuhusu jinsi hatua hiyo itakavyoathiri shughuli za hijja ambazo zinaanza mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Mwaka jana jumla ya waumini milioni 2.5 wa dini ya Kiislamu kutoka pembe zote za dunia walikongamana Saudia Arabia kushiriki hijja, ambayo ni mojawapo ya nguzo tano za dini hiyo.

Vituo vya hajji na Umrah katika mji wa Mecca vinazingirwa na milima na mabonde. Utawala wa Saudia huwa na wakati mgumu kuwashughulikia mamilioni ya waumini ambao husongamana katika maeneo madogo matakatifu.

Misongamano kama hii nyakati zingine husababisha maafa, kama ilivyoshuhudiwa mnamo 2015 ambapo takriban watu 2,300 walifariki.

Ingawa visa vya maambukizi mapya vimesemekana kupungua nchini China ambapo ugonjwa huo hatari ulitokea kwa mara ya kwanza mnamo Desemba mwaka jana, maambukizi yanaongezeka katika maeneo ya bara Asia, Uropa na Mashariki ya Kati.

Tayari watu 15 wamefarik kutokana na ugonjwa huo nchini Iran na kuibua hofu kubwa. Na maambukizi mengine pia yameripotiwa katika mataifa ya Kuwait na Bahrain wiki hii.

You can share this post!

Huu wimbo wa Reggae kamwe haumlengi Ruto – Raila

Kioja abiria jini akipotelea hewani!

adminleo