Michezo

MASIKITIKO! Arsenal yachabangwa 2-1 na Olympiacos

February 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

ARSENAL ilichabangwa 2-1 na Olympiacos na kubanduliwa nje ya Ligi ya Uropa kwa mabao ya ugenini, baada ya mechi ya marudiano ya raundi ya 32 uwanjani Emirates, Alhamisi.

Vijana wa Mikel Arteta walikuwa wamelemea Wagiriki hao 1-0 ugenini mnamo Februari 20. Lakini walizamishwa na bao la Youssef El-Arabi, sekunde 60 kabla ya dakika 30 za nyongeza kutamatika.

Olympiacos ilimaliza muda wa kawaida uwanjani Emirates ikiwa bao 1-0 juu, baada ya Pape Abou Cisse kutikisa nyavu dakika ya 53. Bao lake lilifanya dakika 30 ziongezwe ili kuamua mshindi.

Arsenal ilijipatia matumaini ya kuingia raundi ya 16-bora mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang aliposawazisha 1-1 kupitia bao safi la makasi dakika ya 113.

Bao la Aubameyang liliweka Arsenal mbele 2-1, kwa sababu ilikuwa imeshinda mechi ya mkondo wa kwanza kupitia bao la Alexandre Lacazette.

Hata hivyo, ndoto yao ilizimwa baada ya El-Arabi kupatia Olympiacos bao la pili kunako dakika ya 119.

Aidha, Aubameyang alipoteza nafasi ya wazi sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia.

Kabla ya kichapo hicho, Arsenal haikuwa imepoteza mchuano wowote mwaka huu katika mashindano yote.

Gunners sasa wako katika hatari ya kukosa kabisa mashindano yote ya Bara Ulaya msimu ujao, baada ya kichapo cha Alhamisi.

Katika mechi nyingine usiku huo, mabingwa wa zamani Ajax na Porto pia watasalia kuwa mashabiki tu baada ya kubanduliwa nje katika raundi hiyo ya 32-bora.

Washindi wa 1992, Ajax, ambao waling’ara sana msimu uliopita kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), walichapa Getafe ya Uhispani 2-1 katika mechi ya marudiano nchini Uholanzi.

Lakini waliaga mashindano hayo kwa jumla ya mabao 3-2, kutokana na matokeo ya mkondo wa kwanza walipolimwa 2-0 na Wahispania hao mjini Madrid.

Nao wafalme wa mwaka 2003 na 2011, Porto walikubali vichapo viwili kutoka kwa Bayer Leverkusen na kusalimu amri kwa jumla ya mabao 5-2.

Klabu zingine kubwa zilizofunganya virago kutoka Ligi ya Uropa ni wanafainali Benfica, Sporting Lisbon na Braga kutoka Ureno, Celtic (Scotland) na AZ Alkmaar (Uholanzi).