Uhuru aachia Raila BBI
Na WAANDISHI WETU
SHINIKIZO zinazidi kutolewa kwa Rais Uhuru Kenyatta ajihusishe moja kwa moja na mikutano ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ambayo huongozwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Mikutano ya BBI imeingia kipindi cha lala salama na kaunti zilizosalia kuandaa mikutano hiyo ni ngome za Chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto, mbali na Nairobi.
Mnamo Jumamosi, mkutano wa kaunti za Mlima Kenya ulifanywa katika Kaunti ya Meru ambapo uhalisia wa mgawanyiko wa kisiasa uliopo nchini ulizidi kushuhudiwa.
Mikutano iliyobaki imepangiwa kufanyika katika Kaunti ya Nakuru, Uasin Gishu na Nairobi ilhali Rais Kenyatta hajaonyesha dalili za kuhudhuria mkutano wowote.
Wiki iliyopita, waandalizi wa mkutano wa BBI Meru walikuwa wamesema walimtumia Rais mwaliko.
Lakini Rais alikuwa akikutana na madiwani wa Nairobi katika Ikulu wakati makombora ya kisiasa yalipokuwa yakirushwa katika mkutano huo kati ya viongozi wanaounga mkono BBI na wale wanaopinga, ambao pia ni wandani wa Dkt Ruto.
Ilitarajiwa na wengi kwamba ingekuwa mara ya kwanza mkutano aina hiyo kuhudhuriwa na Rais, Dkt Ruto na Bw Odinga, lakini pia Naibu Rais akakosa kuhudhuria.
Katika Kaunti ya Nakuru ambayo Rais Kenyatta na Dkt Ruto walitumia kutangaza azimio lao la umoja wa kitaifa walipokuwa wakiandamwa na kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) 2013, taharuki imeanza kutanda mkutano wa BBI ukitarajiwa Jumamosi.
Seneta wa Kaunti ya Busia, Bw Amos Wako ambaye ni mwanachama wa jopo la BBI, alisema Jumapili huenda mchakato mzima ukakosa maana ikiwa wanasiasa wataendelea kuruhusiwa kueneza masuala ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 katika mikutano ya hamasisho.
“Inasikitisha kwamba katika midahalo tofauti ya BBI, kinachozungumziwa ni siasa za 2022 kuhusu ni nani atakuwa rais, gavana na nafasi nyinginezo ilhali bado tuna zaidi ya mwaka mmoja kabla uchaguzi ufanywe,” akasema.
Gavana wa Kericho, Bw Paul Chepkwony alisema jinsi hali imegeuka, Rais Kenyatta anafaa atoe mwelekeo kuhusu mikutano hiyo.
“Kama hali hii ya viongozi kueneza chuki itaruhusiwa kuendelea, taifa litaporomoka. Tunamwomba Rais Kenyatta atoe mwelekeo kuhusu suala hili na hata aagize mikutano ikomeshwe,” akasema.
Mkutano wa BBI Nakuru umenuiwa kuleta pamoja Kaunti za Nakuru, Baringo, Bomet, Narok na Kericho.
Rais Kenyatta amekuwa akisifu BBI kama mchakato ambao utaleta umoja wa nchi na kuzuia ghasia za uchaguzi ambazo huathiri maendeleo.
Katika eneo la Kaskazini mwa Rift Valley, kuna tashwishi kuhusu ikiwa mkutano wa BBI utafanyika kaunti ya Uasin Gishu kwani hata tarehe yake haijatangazwa, huku wafuasi wa Dkt Ruto wakisema hawataruhusu mkutano huo kufanyika eneo hilo.
Makundi ya vijana na viongozi wa kidini walisema Rais anafaa kutumia mamlaka yake kukomesha viongozi wanaotumia BBI kueneza chuki na kusababisha vurugu.
“BBI ilinuiwa kuleta umoja wa nchi wala si kugawanya jinsi viongozi wetu wanavyofanya. Sisi kama viongozi wa kidini hatutaruhusu hilo lifanyike,” akasema Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu (SUPKEM) tawi la Kaskazini mwa Rift Valley, Bw Abubakar Bini.
Ripoti za Eric Matara, Onyango K’Onyango, Florah Koech, Gaitano Pessa na Valentine Obara